23.8 C
Dar es Salaam
Monday, September 25, 2023

Contact us: [email protected]

Mvua kubwa zaidi mwishoni mwa wiki

PATRICIA KIMELEMETA

MAMLAKA ya Hali ya Hewa (TMA) imesema mvua kubwa zaidi inatarajiwa kunyesha mwishoni kwa wiki katika maeneo mbalimbali ya nchi na imewataka wananchi kuchukua tahadhari mapema.

Akizungumza na waandishi wa habari  Dar es Salaam jana, Meneja wa Utabiri, Samuel Mbuya alisema mvua hiyo ni mwendelezo wa mvua ya masika  inayoendelea kunyesha maeneo mbalimbali ya nchi baada ya kutonyesha mwezi uliopita kutokana na kuwapo  kimbunga Kenneth ambacho kilibadili hali ya hewa.

Alisema kutokana na hali hiyo, wananchi wanapaswa kuchukua tahadhari mapema huku wakiendelea kufuatilia taarifa za hali ya hewa   waweze kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza.

“Mwishoni mwa wiki hii tunatarajia kupata mvua kubwa zaidi katika maeneo mbalimbali ya nchi yanayopata mvua za masika, hivyo basi ni muhimu kwa wananchi kuchukua tahadhari mapema,”alisema Mbuya.

Mbuya alisema  juzi kituo cha kupima mvua cha Pemba kilionyesha kiasi cha mvua ni milimita 105.3 wakati jana iliongezeka na kufikia milimita 181.0.

Alisema  kituo cha kupima mvua kilichopo Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA), juzi kilipima kiasi cha mvua kuwa milimita 64.4 na jana iliongezeka hadi kufikia milimita 79.0, wakati Zanzibar ilionyesha 127.3.

Alisema kutokana na hali hiyo  mvua itakayonyesha mwishoni mwa wiki  inaweza kufikia kiwango hicho au kuongezeka zaidi hasa katika Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga, Zanzibar na Pemba.

Alisema Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini na Mikoa ya Kanda ya Ziwa itaendelea kupata mvua ya masika kama kawaida, hivyo basi wakulima wanapaswa kufuatilia taarifa za hali ya hewa.

Barabara zafunguwa kwa muda

Kutokana na mvua ya juzi na jana, Jeshi la polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam  lililazimika kufunga barabara ya Morogoro eneo la Jangwani baada ya mto Msimbazi kujaa maji.

Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Marson Mwakyoma, alisema eneo hilo lilisababisha kutenganisha barabara kati ya wakazi wa Jangwani na Magomeni, jambo ambalo linaweza kusababisha maafa.

“Jeshi la polisi limelazimika kufunga barabara kipande cha Magomeni na Jangwani baada ya eneo la Jangwani kujaa maji na kupita juu ya daraja, jambo ambalo lingeweza kusababisha maafa,”alisema Kamanda Mwakyomba.

Alionyesha pia kushangazwa na baadhi ya madereva wa bajaji na bodaboda ambao walikuwa wakivusha wananchi katika eneo hilo.

 “Wananchi sijui wana shida gani, hivi hawawezi kufikiria mpaka wasubiri polisi wawakamate?

“Nimeshangaa kuona bodaboda imebeba abiria na kuwavusha eneo la Jangwani wakati maji yamejaa bila kuogopa wala kuwa na wasiwasi kuwa wanahatarisha maisha yao,”alisema.

Alisema kutokana na hali hiyo, Jeshi la Polisi limeimarisha ulinzi katika eneo hilo kwa kuweka askari upande wa Jangwani na Magomeni   kuangalia usalama wa eneo hilo wakati huu ambao limewekwa zuio hilo.

Alisema ikiwa maji yatapungua  uzio huo ungeondolewa na kuruhusu magari kupita  yaweze kuendelea na shughuli z kama kawaida.

Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart) walisema walirudisha huduma ya usafiri wa mabasi hayo baada ya eneo la Jangwani kupungua maji.

Baadhi ya wananchi waliozungumza na gazeti hili walisema mvua iliyonyesha katika maeneo ya Jangwani ilisababisha usumbufu wa usafiri katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam.

“Tunapanda bajaji kutoka Mbezi hadi Magomeni kwa Sh 6,000 wakati awali tulikua tunapanda kwa Sh 1,000 mpaka Kariakoo,”alisema Shadrack mkazi wa Mbezi Luis.

Alisema  hali ya usafiri ilikua ngumu  jambo ambalo liliwafanya wananchi kukubali kulipa kiasi hicho cha fedha  waweze kwenda kazini.

Naye mkazi wa Kimara, Amina Issa alisema  hali ya usafiri ilikua ngumu kutokana na mvua inayoendelea kunyesha, jambo ambalo lilisababisha usumbufu kwa abiria.

“Magari yamepandisha gharama za usafiri tofauti na zamani  jambo ambalo limetufanya sisi tusiokua na uwezo kutembea kwa miguu kutoka Kimara hadi Magomeni kwenda Kariakoo,” alisema Amina.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,718FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles