MVIWATA WAMWUNGA MKONO JPM

0
642

Na Lilian Justice-MorogoroMTANDAO wa vikundi vya wakulima Tanzania (MVIWATA) umetoa tamko la kumwunga mkono Rais Dk. John Magufuli kwa jitihada zake za za kupigania rasilimali za taifa hususani madini.

Hayo yalisemwa jana na Mwenyekiti wa Mtandao huo, Veronica Sophu wakati akitoa tamko la kuunga mkono jitihada hizo kwa niaba ya wakulima kwenye kongamano lililofanyika mjini Morogoro.

Sophu alisema kuwa MVIWATA inamwunga mkono Rais Magufuli kwa jitihada mbalimbali anazozifanya na kwamba wakulima wote wako nyuma yake na kamwe asifikiri vita ya uchumi anayoifanya yuko peke yake.

“Sisi wakulima tuko pamoja na Rais Magufuli kwa kile anachokifanya tunamwomba asikatishwe tamaa na wale wachache wasiopenda maendeleo wanaotaka kutunyang’anya rasilimali zetu,’’alisema Sophu.

Aidha alisema kuwa MVIWATA inaunga mkono hatua zote za kuhakikisha kwamba rasilimali za nchi zinawanufaisha watanzania wote na hasa wa tabaka la chini hivyo wakulima wanatambua kuwa vita iliyoanzishwa na Rais Magufuli ni ngumu na inahitaji mshikamano wa kitaifa wa Watanzania .

‘’Hii ni vita ya kupigania uhuru wa kiuchumi na hivyo ni ngumu na ina maadui wengi na ndio maana tumekusanyika hapa wakulima ili kutuma ujumbe kwamba jemedari wetu hayupo peke yake , sisi sote tupo nyuma yake,’’alisema Mwenyekiti huyo.

Awali akifungua kongamano hilo, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk. Kebwe Stephen Kebwe alisema wakulima wameonyesha moyo wa uzalendo kwa kuonyesha hisia zao dhidi ya Rais Magufuli na kuunga mkono kwa vitendo.
Kebwe alisema kuwa jitihada hizo zinaonekana ndani na nje ya nchi na kuwataka wakulima nchini kutambua kuwa wao ndio wazalishaji wakuu wa Taifa na kuwataka kuongeza zaidi uzalishaji.

Naye Mkurugenzi wa Mtandao wa vikundi vya wakulima Tanzania (MVIWATA), Stephen Ruvuga alisema kuwa lengo la kongamano hilo ni kuunga mkono hatua zote Rais Magufuli anazozichukua za kupigania rasilimali za nchi.

“Sisi kama jumuiya ya wakulima tunaonyesha hisia zetu kwa Rais Magufuli kuwa hatuko nyuma bali tuko bega kwa bega na y eye kwa kile anachokifanya kwa ajili ya kuliletea taifa maendeleo,” alisema Ruvuga.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here