28.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, March 22, 2023

Contact us: [email protected]

Mv Mwanza Hapa Kazi Tu kuingizwa majini kesho kwa mara ya kwanza

Na Clara Matimo, Mwanza

Meli ya Mv Mwanza Hapa kazi Tu inayojengwa katika bandari ya Mwanza Kusini iliyopo Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza kwa gharama ya zaidi ya Sh bilioni 108 kesho Februari 12, 2023 itaingizwa kwa mara ya kwanza ndani ya maji ili kujaribiwa.

Meli  hiyo ambayo ikikamilika itakuwa na uwezo wa kubeba abiria 1,200 na tani 400 za mizigo, itafanya safari zake katika nchi zote ambazo ziko ukanda wa ziwa viktoria.

Akizungumza na waandishi wa habari  katika ukumbi uliopo ofisi ya Mkuu wa Mkoa  wa Mwanza leo Februari 11, 2023, Mkuu wa Mkoa huo, Adam Malima amesema kuitoa meli nchi kavu na kuiingiza ndani ya maji ni hatua ya pili kubwa kwenye ujenzi wa chombo chochote cha ndani ya maji .

Malima amesema meli hiyo ikianza kufanya safari zake itakuwa ni chachu ya kuleta uchumi nchini hasa kwa wakazi wa  mikoa ya kanda ya ziwa  pia wananchi wataweza kusafiri kwa kutumia gharama nafuu.  

“Tunamshuku sana Dk. Samia Suluhu Hassan kwa usimamizi wa miradi ya kimkakati ya namna hii ukiwemo huu wa meli na hatua tuliyofikia ambayo ni kubwa sana, wakati  serikali ya awamu ya sita inaingia madarakani ujenzi wa meli hiyo ulikuwa umekamilika kwa asilimia 45 sasa umefikia asilimia 82.

“Pia tunamshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye ametusaidia sana kumaliza mkwamo uliokuwepo baina ya serikali na mkandarasi ambaye ni kampuni ya GAS Entec ya Korea Kusini sasa ujenzi unaendelea vizuri sana tunatarajia  hadi kufikia  Juni mwaka huu itaanza kutoa huduma,”ameeleza Malima

Mkurugenzi Mtendaji wa MSCL, Mhandisi  Eric Hamissi amesema kesho chuma chenye takribani uzito wa tani 3,000 kitaingizwa ndani ya maji  ambapo amefafanua kwamba meli hiyo ikikamilika ujenzi wake itakuwa na uzito wa tani 3,500.  

Amesema meli hiyo ya MV Mwanza Hapa Kazi Tu ina urefu wa mita 92.6, kimo ghorofa nne, upana mita 17 pia itakuwa na mwendo kasi tofauti na zingine zote ambazo zinafanya safari zake katika maziwa makuu hivyo itarahisisha  shughuli  za usafiri na usafirishaji kwa abiria na mizigo.

Mhandisi Hamissi ametaja sifa za meli hiyo kwamba itakuwa na madaraja sita, itaweza kubeba viongozi wakuu wa kitaifa wawili, VIP nne, first class 60, business class 100, second class 200, wasafiri wa kawaida 834, inaukumbi wenye uwezo wa kubeba watu 400 ambao wanaweza kufanyia sherehe humo kwa hivyo itakuwa ni kivutio kizuri sana,” ameeleza Mhandisi Hamissi.

Mwenyekiti wa Bodi ya MSCL, Meja Jenerali Mstaafu John Mbungo aliishukuru serikari ya awamu ya sita kwa uwekezaji mkubwa inaoufanya katika miradi ya kimkakati ambayo imelenga kuwanufaisha wananchi ukiwemo wa meli ya Mv Mwanza Hapa Kazi Tu.

“Tukio la kesho ni kubwa sana wananchi wajitokeze kwa wingi waje washuhudie  tukio hilo ambalo ni kubwa sana kwa taifa na mkoa wa Mwanza,”amesema Meja Jenerali Mstaafu Mbungo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,079FollowersFollow
563,000SubscribersSubscribe

Latest Articles