24.8 C
Dar es Salaam
Friday, October 4, 2024

Contact us: [email protected]

MUWSA yapongezwa kuwa mamlaka bora ya maji

Jacquiline Mrisho – MAELEZO

SERIKALI imeipongeza Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mjini Moshi (MUWSA) kwa kuwa mshindi wa jumla kati ya mamlaka nane zilizoshindanishwa na Jumuiya ya Taasisi za Udhibiti wa Sekta ya Maji zilizopo katika nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika (ESAWAS).

Pongezi hizo zimetolewa hivi karibuni jijini Dodoma na Katibu Mkuu, Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Profesa Kitila Mkumbo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuipongeza mamlaka hiyo kwa kufanya vizuri katika shindano hilo.

Hii ni mara ya nne tangu mashindano hayo yaanze kufanyika.

Profesa Kitila alisema katika mchakato huo, Taasisi ya ESAWAS ilishindanisha mamlaka moja bora kutoka kila nchi wanachama na kupata mshindi wa jumla kwa mwaka wa fedha wa 2016/17 ambapo kwa Tanzania mamlaka bora katika kutoa huduma ya maji mwaka 2016/17 ilikuwa MUWSA.

“Katika kikao cha mkutano mkuu (AGM) kilichofanyika Novemba 2018, taasisi hii iliitangaza rasmi MUWSA kuwa mshindi wa jumla kwa kupata asilimia 79.9  ikifuatiwa na WASAC ya Rwanda kwa asilimia 77.4 na Nyeri ya Kenya asilimia 70.8.

“Hivyo wizara inaipongeza MUWSA kwa kazi nzuri katika kutoa huduma ya maji na tunaamini itakuwa kichocheo kwa mamlaka nyingine za maji kuongeza juhudi,” alisema Profesa Kitila.

Alivitaja vigezo vitatu vilivyotumika kushindanisha mamlaka hizo kuwa ni ubora wa huduma, ufanisi wa kiuchumi na uendelevu wa mtoa huduma na MUWSA imekuwa mshindi wa kwanza katika eneo la uendelevu wa huduma kwa kupata asilimia  94.6.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa MUWSA,  Joyce Msiru, alisema mafanikio ya ushindi huo yametokana na ushirikishwaji mkubwa wa wadau na bodi ya mamlaka hiyo kwa asilimia 100 kwani Manispaa ya Moshi ina maji yenye ubora wa hali ya juu katika kila eneo.

“Upatikanaji wa maji safi na yenye ubora wa hali ya juu katika maeneo yote ya Manispaa ya Moshi ndio unaofanya hata manispaa hiyo kuwa jiji safi kuliko majiji mengjne nchini,” alisema Joyce.

Jumuiya ya Taasisi za Udhibiti wa Sekta za Maji zilizopo katika nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika inaundwa na nchi za Kenya, Msumbiji, Rwanda, Tanzania, Lesotho, Zambia, Burundi na Zanzibar.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles