25.5 C
Dar es Salaam
Thursday, September 28, 2023

Contact us: [email protected]

MUWEKE WAZI MWANAO MAENEO MUHIMU ASIYOPASWA KUSHIKWA

Na Christian Bwaya


MATUKIO ya watoto kudhalilishwa kijinsia yanazidi kuongezeka. Tumesikia taarifa za watoto wadogo kubakwa, kulawitiwa, kutomaswa kingono, kushikwa shikwa miili yao na watu wazima na wakati mwingine watoto wenzao.

Katika matukio yanayodaiwa kutokea hivi karibuni, tunaambiwa mwalimu aliyekuwa karibu na wanafunzi ndiye aliyekuwa na tabia ya kuwanyanyasa kingono. Unaweza kujiuliza kwanini watoto hawa wanyanyaswe kingono na bado wakae kimya? Kwanini hawakusema?

Ukifuatilia matukio haya ya udhalilishaji wa watoto, utagundua kuwa mara nyingi yanafanywa na watu walio karibu na mtoto, ambao kwa hali ya kawaida, mtoto anawaamini. Hapa tunazungumzia walimu, wajomba, ndugu wa karibu kwenye familia, marafiki ambao mtoto hawezi kuwa na wasiwasi nao.

Unaweza kuona kwanini watoto hawa wanaodaiwa kuwa wahanga wa vitendo vya udhalilishaji vilivyokuwa vikifanywa na mwalimu wao, hawakuwa na ujasiri wa kusema kwa mtu yeyote kwa sababu pamoja na mambo mengine, aliyekuwa anawafanyia vitendo hivi ni mtu waliyekuwa na imani naye.

Katika mazingira ya ukaribu wa namna hii, inakuwa rahisi kwa mtoto kufika mahali akaamini kuwa kile anachokifanya na mtu anayemwamini kama mwalimu wake ni kitu cha kawaida na hivyo hakuna sababu ya kukisema kwa wengine.

Unaweza kuuliza, kwanini mtoto akubali kushikwa shikwa na mtu na bado asitoe taarifa kwa wazazi au walimu wengine? Usiwe mwepesi kumlaumu mtoto.  Ukitazama kwa makini unaweza kuona na sisi wazazi tunachangia tatizo kwa sababu hatuwafundishi umuhimu wa kuwa na mipaka wanapokuwa na watu wengine. Mtoto anashikwa sehemu za mwili wake na hastuki. Na kwa sababu anayemfanyia hivyo ni mtu anayemwamini, inakuwa vigumu kuelewa hatari inayofuata kwa sababu hajafundishwa mipaka.

Nina mapendekezo matatu. Kwanza, wazazi tuwe karibu na watoto. Tunahitaji kuweka mazingira ambayo mtoto anakuwa na imani na sisi kuliko mtu mwingine yeyote. Kipimo kuwa mtoto anakuamini ni utayari wake wa kukuambia mambo anayokutana nayo kila siku. Anaporudi nyumbani atakueleza amekutana na nani, amefanya nini, na wakati mwingine hatakuwa na wasiwasi kuelezea hata makosa aliyoyafanya huko alikokuwa. Katika mazingira kama haya, ni vigumu mtoto kukutana na kitu kisicho cha kawaida na kisifahamike kwako mzazi.

Lakini hatua ya pili ninayoipendekeza ni wazazi kuwafundisha watoto umuhimu wa kuwa na mipaka katika uhusiano wao na watu. Mahali pa kuanzia, mathalani, ni kutokuingia kwenye chumba cha wazazi bila ruhusa. Lazima abishe hodi aruhusiwe kuingia. Tunapoweka uholela nyumbani, kiasi kwamba mtoto anaweza kuingia kokote bila ruhusa tunajenga mazoea ya hatari.

Sambamba na hili, watoto waelewe umuhimu wa faragha katika maisha. Haifai, kwa mfano, kuvua nguo mbele za watu, kumruhusu mtu yeyote kumshika maeneo fulani ya mwili, kukaa maeneo fulani na watu na mambo yanayofanana na hayo. Mtoto aliyefundishwa mipaka hii ya maisha atabaini kirahisi anapokutana na mtu mwenye nia ovu.

Vilevile, tuwawekee watoto mazingira ya kuwaripoti watu wanaowafanyia tabia zisizo za kistaarabu hata kama ni watu walio karibu naye. Ili hili liwezekane, tusiwe wepesi kuwahukumu watoto kwa sababu tu wameeleza jambo lililowatokea na hatulipendi. Unapokimbilia kumwadhibu mtoto unamfundisha kuepuka adhabu kwa kuficha baadhi ya mambo.

 

Christian Bwaya ni Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Twitter: @bwaya, Simu: 0754870815

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,750FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles