Michael Andendekisye, Dar es salaam
KWA wasomaji wa vyombo vya habari hapa nchini, katika masuala ya uwekezaji taarifa iliyokuwa ikiandikwa sana katika siku za karibuni ilihusu mgogoro uliokuwepo baina ya kampuni ya Acacia na Barrick Gold.
Ni rahisi sana, katika mazingira ya namna hii, watu kusahau kuhusu manufaa mengi ambayo sekta binafsi na wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi wameiletea nchi yetu katika kipindi cha miaka 20 iliyopita.
Sitakwenda mbali sana na ukweli kama nitasema kwamba kama kuna mbia mkuu wa serikali katika mafanikio yote ya kiuchumi ambayo Tanzania imeyapata kwa zaidi ya miongo miwili iliyopita, basi mbia huyo ni sekta binafsi.
Mfano mmoja wa wazi kuhusu mchango wa sekta binafsi ambao mtu anaweza kuuona kwa uwazi kabisa ni ule wa sekta ya mawasiliano. Hakuna Mtanzania mtu mzima ambaye hajawahi ama kutumia simu kwa maongezi au kupitia huduma zake za mtandao na zile za kifedha.
Jambo hili limebadilisha maisha ya mamilioni ya Watanzania ambao sasa wanajiuliza waliokuwepo miaka 50 au 40 iliyopita waliwezaje kumudu maisha yao pasipo simu.
Kampuni na wawekezaji hawa katika sekta binafsi kwenye sekta ya mawasiliano wamefanya kazi kubwa katika kuwekeza mitaji yao ili kuhakikisha kwamba mamilioni ya Watanzania wanaunganishwa katika huduma za simu.
Mchango huu wa sekta hii umekuwa mkubwa na ukikua –kiasi kwamba sasa Tanzania ina jumla ya kampuni za simu nane; idadi inayoelezwa kuwa ya juu miongoni mwa nchi za Afrika zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Idadi hiyo imekuwa kubwa kiasi kwamba maswali yameanza kuulizwa endapo idadi hii ya kampuni nane za simu ndani ya nchi yetu ni jambo sahihi. Katika hali ya kawaida, mtu angeweza kusema kwamba kuwa na kampuni nyingi ni jambo la heri. Kwa bahati mbaya, hali haiku hivyo kwa kwenye tasnia ya mawasiliano.
Uzoefu na tafiti mbalimbali zilizowahi kufanyika katika miaka ya karibuni unaonyesha kwamba wakati namba ya washindani katika sekta hii inapokuwa ndogo, uwezekano wa kuongeza uwekezaji ni mkubwa kuliko kampuni zikiwa nyingi.
Wakati idadi ya washindani ikiwa ndogo, kampuni hizi hupata faida nzuri; jambo linaloziwezesha kufanya uwekezaji katika utafiti na masoko, ambalo baadaye huboresha zaidi huduma kwa wateja.
Naweza kutoa mfano mmoja wa kufikirika kuhusu umuhimu wa kampuni mbili au zaidi za simu kuungana na kutengeneza moja.
Kila kampuni huwa na bidhaa yake moja ambayo huwavutia wateja kwake. Zinapoungana kampuni mbili, maana yake ni kwamba wateja wa kampuni hizi sasa watapata huduma zote za kampuni zilizoungana kabla hazijaungana.
Hii maana yake ni kuwa wateja hufaidika kwa fedha yao kuwa na thamani zaidi kuliko ilivyokuwa kabla ya kuungana. Kama mtandao mmoja ulikuwa umejikita zaidi mijini na mwingine vijijini, mteja sasa atajikuta yuko katika mtandao unaosikika vema mijini na vijijini –huku akitumia kiasi kilekile cha fedha alichokuwa akitumia zamani.
Hadi sasa, sekta binafsi inaendelea kutoa mchango mkubwa sana katika ukuaji wa uchumi wetu na kutoa fursa kwa maelfu ya vijana wanaotafuta fursa za kiuchumi.
Tukitazama mbele, pamoja na migogoro ya hapa na pale miongoni mwa wadau muhimu katika sekta binafsi, mustakabali wa taifa letu kiuchumi una mwelekeo mzuri.
Kinachotakiwa ni kuzidi kuboresha mapungufu yaliyopo, ikiwamo kuchagiza kampuni za mawasiliano ziungane, ili hatimaye kasi ya kusukuma mbele uchumi wetu iwe ya kubwa na isiyo na mushkeli.