25 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 8, 2021

Mutungi: Tunataka kumaliza vyama vya mfukoni

GRACE SHITUNDU -DAR ES SALAAM

MSAJILI wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, amevitaka vyama vinavyohofia kufutwa kutokana na uhakiki wa vyama unaotarajiwa kufanywa na ofisi hiyo kuanzia Machi 17, viondoe hofu kwani lengo ni kuondoa vyama vya mfukoni.

Akizungumza na viongozi wa vyama hivyo Dar es Salaam jana, Jaji Mutungi alisema lengo la uhakiki huo ni kufanya tathmini ya vyama ili kuondokana na dhana ya kuwepo chama cha mfukoni. 

“Kazi ya uhakiki ni moja ya majukumu yanayofanywa na ofisi ya msajili na kazi ya chama ni kutunza uhalali wake, kuhakikisha kinakuwa hai, hivyo tunapofanya uhakiki ni kujiridhisha.

 “Zoezi hili halina nia ya kutaka kufuta chama chochote, bali ni kufanya tathmini na kuangalia endapo vyama vilivyopo vina vigezo vyote vinavyohitajika,” alisema Jaji Mutungi.

Akizungumza lengo la kikao hicho, Jaji Mutungi alisema ni kuwajulisha mapema zaidi kuhusu uhakiki huo.

“Tunachojaribu kuwaeleza hapa ni kuwaweka tayari, isiwe kama dereva wa daladala akimuona askari ndio anafunga mkanda akiondoka anafungua, tunataka kuwasaidia ninyi muwe na mahali pazuri pa kufanyia kazi zenu za chama,” alisema Jaji Mutungi.

Alisema ofisi yake inataka vyama hivyo vijiendeshe kama taasisi kamili.

“Tunataka vyama vya siasa vijiendeshe kama taasisi, kuna wakati wenyewe kwa wenyewe mnakosana, basi mmoja wenu anafunga ofisi na nyaraka muhimu za chama unakuta zipo ndani, shughuli zote za chama zinasimama,” alisema Jaji Mutungi.

Naye Naibu Msajili vya Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza, alisema katika zoezi hilo watapita kufanya uhakiki katika ofisi zote za makao makuu ya chama na ofisi ndogo, Bara na Visiwani.

“Zoezi la uhakiki limepangwa kuanza Machi 17 mwaka huu na tutapita katika ofisi zote za vyama, makao makuu na ofisi ndogo, chama chochote cha siasa kinapaswa kuwa na ofisi kuu na ndogo hapa Tanzania Bara na Visiwani,” alisema Nyahoza.

Alisema uhakiki huo hautaishia katika ofisi kuu pekee, bali utaendelea kwenye ofisi za mikoa na wilaya.

“Uhakiki wetu hautaishia katika ofisi kuu peke yake, kuna siku tutaamua kwenda mkoani kuangalia kama chama chenu kipo, kwani ni lazima chama kiwe na orodha ya wanachama katika ngazi mbalimbali mkoa, wilaya au jimbo,” alisema Nyahoza.

Akizungumzia mambo mengine watakayofanyia uhakiki ni pamoja na kuangalia orodha ya mali na vifaa vya chama. 

“Rejista ya samani au mali za chama, kitu chochote cha chama kisajiliwe kwa jina la chama, kwani inawezekana mtu akanunua kochi kwa ajili ya ofisi, mwisho wa siku wakikorofishana anaanza kudai ofisi kochi lake,” alisema Nyahoza.

Pia alisema kuhakikisha chama kinakuwa na akaunti maalumu ambayo fedha zinapitia huko ili kuweka kumbukumbu ya mapato na matumizi.

“Kwa vile vyama ambavyo vinapokea ruzuku vinatakiwa kuwa na akaunti mbili ambapo fedha za ruzuku zisichanganywe na zile zinazotokana na vyanzo vingine ili kuhakikisha fedha hizo zinatumika kwa mambo yanayohusu fedha ya ruzuku tu,” aliongeza Nyahoza.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
168,540FollowersFollow
527,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles