27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Muswada wa Habari wawatifua Zitto, Nape

zittokabwe

Na MWANDISHI WETU- DAR ES SALAAM

MUSWADA wa Sheria wa Huduma za Habari Mwaka 2016 umeibua malumbano na mjadala wa hoja kinzani kati ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye na Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe.

Kwa siku mbili mfululizo, Nape na Zitto wametumia jukwaa la mitandao ya kijamii kutifuana kuhusu muswada huo unaotarajiwa kuwasilishwa katika Bunge lijalo linalotarajiwa kuanza mwezi ujao.

Katika ujumbe wa maandishi wa kumjibu Zitto alioutuma Nape katika mtandao wa jamii, alimlaumu Zitto kuwa anajaribu kupotosha jamii kuhusu masuala kadhaa yanayohusiana na muswada huo.

“Naona juhudi kubwa za Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, kujaribu kupotosha jamii kwa kutosema ukweli kuhusu masuala kadhaa yahusianayo na Muswada wa Huduma za Habari, 2016. Kwa kawaida mimi huwa si mtu wa kujibu hoja zinazotolewa kinafiki na kioga kama alivyofanya rafiki yangu Zitto. Kwa hali ya kawaida ningeweza kumpuuza kabisa, lakini kwa hili uvumilivu wangu kwa kiwango hiki cha unafiki umefikia ukingoni. Hivyo nitalazimika kujibu baadhi ya hoja,” alisema Nape kupitia andishi lake.

Aliitaja hoja ya kwanza ya ushiriki wa wadau na alimlaumu Zitto kwa kujenga picha kuwa haujashirikisha wadau na wakati anajua wazi kuwa katika utungaji wa muswada kuna hatua mbili za kutoa maoni.
“Hatua ya kwanza ni pale ambapo Serikali inapokuwa inatengeneza muswada husika kabla ya kuupeleka kwenye vikao vya kiserikali kwa hatua za kuupitisha wadau hushirikishwa ili kutoa maoni yao. Na kwa muswada huu, wadau wameshirikishwa tena na ushahidi wa maandishi wa ushiriki wao na maoni yao upo.

“Hatua ya pili ya utoaji maoni huwa ni baada ya muswada kusomwa mara ya kwanza bungeni, muswada husika hukabidhiwa kwa kamati husika ya Bunge na ukishakabidhiwa huwa ni waraka huru kwa umma kuusoma na kutoa maoni yao (public document) kwa Kamati ya Bunge.

“Hili pia limefanyika hadi hatua ya wadau kuitwa na kuja Dodoma ambapo waliomba mbele ya kamati wapewe muda wakamilishe kazi ya kusoma na kutoa maoni yao. Na Mwenyekiti wa Kamati, Peter Serukamba, kwa uamuzi wa Kamati ya Kudumu ya Bunge wakaamua kuwaongezea muda wadau kwa wiki moja kukamilisha kazi hiyo, shughuli inayoendelea sasa,” alisema.

Nape alijibu hoja ya pili inayohusu vyombo vya habari kujiunga na Shirika la Taifa la Utangazaji (TBC) kwa kumlaumu Zitto kwa kunena uongo kwamba muswada huo unadhamiria kuvifanya vyombo hivyo hususani televisheni kulazimishwa kujiunga na TBC katika vipindi vyake.

“Hakuna kifungu kama hicho katika muswada huu; pili, hakuna dhamira hiyo katika muswada huu na tatu Serikali haina hata wazo hilo,” alisema.

Kuhusu hoja ya mitandao ya kijamii, Nape alisema Zitto kapotosha juu ya suala hilo kwa kusema kuwa muswada unakusudia kuzibana blogu na kutaja mitandao ya kijamii kama JamiiForums.

Kuhusu hoja ya mamlaka ya waziri kuzuia chapisho au kitabu fulani kisisambazwe, Nape alikiri ukweli ingawa alimtuhumu Zitto kwa kutoweka ukweli wote juu ya madai yake.

“Muswada unampa waziri mamlaka hayo si kwa kila jarida au kitabu bali yale tu ambayo yamedhihirika kuchapisha habari huku yakivunja sheria za nchi. Kama Zitto anafikiri nchi yetu itaruhusu majarida yanayotaka kuhamasisha vita na uvunjifu wa amani nchini, ajue hakuna nchi inayoruhusu mambo hayo,” alisema.

Baada ya Nape kutoa hoja hizo, Zitto naye akamjibu kupitia akaunti yake ya Mtandao wa Facebook.

Zitto alianza kwa kusema: “Ndugu yangu Nape Nnauye amejibu andiko langu nililolitoa jana (juzi) kuhusu muswada tajwa. Kama ilivyo ada ya siasa za kijinga jinga Nape amejibu andiko langu kwa kunishambulia binafsi na kuweka hoja zake mbalimbali. Mimi sitamjibu Nape namna yake maana wenye busara wametufunza; ‘when they go low go high’. Nitajibu hoja za Nape na sitamjibu Nape. Hata katika andiko langu sikutamka neno Nape Nnauye kwani siasa zangu si siasa za mtu bali za masuala. Sitahangaika na mtu bali hoja ili kujenga,” alisema.

Zitto alianza na hoja ya kushirikishwa wadau kwa kusema kanuni za Bunge (kanuni ya 84) zinataka muswada ukishasomwa kwa mara ya kwanza, Bunge linatakiwa kufanya matangazo kwa umma ili kuhakikisha kuwa umma unaelewa maudhui ya muswada na kuwezesha wananchi kutoa maoni yao.

“Muswada huu kwanza Bunge halikutoa matangazo yoyote (kwa taarifa tu ni kwamba hata Kamati ya Bunge ilishindwa kutoa photocopy nakala za uchambuzi wa muswada kutoka kwa wanasheria wa Bunge kwa sababu Bunge halina fedha,” alisema.

Akizungumzia hoja ya kulazimisha vyombo vya habari nchini kujiunga na TBC, alisema itakumbukwa kuwa muswada wa awali ulikuwa na kifungu hicho na wadau wakapiga kelele kukataa.

“Ukisoma muswada huu kwa juu juu utaweza kuona kuwa kifungu hiki hakipo. Mtu mwenye dhamira ovu huficha mambo yake. Katika muswada huu mambo mengi yaliyokataliwa na wadau sasa yamewekwa kiujanja ujanja kwa kuweka mamlaka hayo kwa waziri mwenye dhamana ya habari.

“Serikali inaposema hakuna kifungu hicho haisemi kuna kifungu gani. Nitawaeleza kifungu kilichowekwa ambacho ndicho kitatumika na waziri kufanya haya bila kuhojiwa na mtu yeyote yule, kupitia kanuni. Sehemu ya 7(1) (b)(iv) inatamka wazi kwamba waziri anaweza kuagiza chombo chochote cha habari cha binafsi kutangaza habari fulani au masuala fulani yenye umuhimu kwa Taifa,” alisema.

Akijibu hoja ya mitandao ya kijamii, Zitto alisema muswada uliopo mbele ya Kamati ya Bunge unatoa tafsiri pana ya vyombo vya habari.

Alisema sehemu ya tatu ya muswada inatamka chombo cha habari yakiwamo magazeti, vituo vya redio na televisheni pamoja na mitandao ya kijamii (online platforms).

“Napenda umma wa Watanzania ufahamu kwamba muswada ni wa Kiingereza. Muswada wa Kiswahili ni kwa ajili tu ya kuwezesha wabunge wasiojua Kiingereza kuweza kuelewa vifungu vya muswada. Muswada ni wa Kiingereza, ndiyo rasmi. Mahakamani hawatatumia muswada wa Kiswahili bali muswada rasmi na tafsiri ya online platforms haikuwekwa katika muswada. Tafsiri ya media ndiyo imeweka hilo la online platforms. Naomba mtu yeyote aende google na kuandika online platform atapata tafsiri ni nini,” alisema Zitto.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles