25.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Muswada Mahakama ya mafisadi watua bungeni

Bunge-1Na Khamis Mkotya, Dodoma

SERIKALI imepeleka bungeni Muswada wa Marekebisho ya Sheria mbalimbali ikiwamo Sheria ya Uhujumu Uchumi inayolenga kuanzishwa  Divisheni ya Mahakama Kuu itakayoshughulikia makosa ya rushwa na uhujumu uchumi.

Kwa mujibu wa muswada huo, mahakama hiyo itakua na mamlaka ya kusikiliza mashauri yote yanayohusu uhujumu wa uchumi bila kujali thamani yake, wakati kwa makosa ya rushwa itasikiliza mashauri yenye thamani isiyopungua Sh bilioni moja.

Muswada huo wa mwaka 2016 uliosomwa bungeni kwa mara ya kwanza, unapendekeza kufanya marekebisho katika sheria tano.

Pamoja na sheria hiyo ya uhujumu uchumi sura ya 200, pia kuna sheria ya Mamlaka ya Rufaa sura ya 141,  Sheria ya Usimamiaji Haki na Matumizi ya Sheria sura ya 358 (JALA).

Nyingine ni Sheria ya Mahakama ya Mahakimu, sura ya 11 na Sheria ya Rufaa za Kodi sura 408, ambako mapendekezo ya marekebisho hayo ni kuondoa upungufu ambao umejitokeza katika sheria hizo wakati wa utekelezaji wa baadhi ya masharti katika sheria hizo.

Katika sheria ya uhujumu uchumi, pia marekebisho yake yanalenga makosa ya uhujumu uchumi bila kujali thamani yake   na muundo, mamlaka na utekelezaji wa mahakama hiyo inayopendekezwa.

Masuala ya kuzuia ufilisi, mamlaka ya Jaji Mkuu kutengeneza kanuni na makosa ya rushwa na uhujumu uchumi, ni mambo yaliyozingatiwa katika sehemu hiyo.

Pia masharti yaliyomo kwenye sheria ya usalama wa mashahidi, sura ya 446 yanapendekezwa kutumika katika masuala yanayohusiana na usalama wa mashahidi kwa kukifanyia marekebisho kifungu 53.

Masuala mengine yanayopendekezwa yanahusu utaratibu wa kuwafikisha watuhumiwa kwenye divisheni, utoaji wa dhamana na adhabu  na utaratibu wa kukata rufaa.

Kuhusu Sheria ya Mamlaka ya Mahakama ya Rufaa, kifungu cha 4 kinarekebishwa kwa madhumuni ya kuipa mahakama ya rufaa mamlaka ya  sheria ya kupitia upya uamuzi wake wa awali pale ambako ni lazima na muhimu kufanya hivyo.

Mahakama hiyo kwa sasa inatekeleza mamlaka hayo kwa kupitia uamuzi wa Mahakama na Kanuni za Mahakama ya Rufaa za mwaka 2009.

Katika Sheria ya Usimamiaji Haki na Matumizi ya Sheria, marekebisho hayo yanapendekeza kuongeza kifungu kipya cha 4 A   kumwezesha Jaji Mkuu kuanzisha Divisheni za Mahakama Kuu   itakapohitajika kwa lengo la kutekeleza majukumu mbalimbali ya kimahakama kama itakavyoamuliwa na Jaji Mkuu.

Kuhusu Sheria ya Mahakama ya Mahakimu, Kifungu cha 18(i)(ii) kinarekebishwa kwa lengo la kuongeza thamani ya mashauri ya madai yanayosikilizwa na mahakama ya mwanzo kutoka Sh milioni tano na kuwa Sh milioni 50.

Hata hivyo katika muswada wa sheria ya marekebisho ya sheria mbalimbali sehemu ya pili inalenga kufanyika katika sheria 20.

Sheria hizo ni Sheria ya kudhibiti utakatishaji wa fedha haramu sura ya 423, Sheria ya kuzuia usafarishaji wa binadamu, sura ya 432, Sheria ya kanuni za madai sura ya 33, Sheria ya usajili wa makandarasi sura ya 235, Sheria ya Elimu sura ya 353, Sheria ya taasisi za kazi sura ya 300, Sheria ya ushahidi sura ya 6 na Sheria ya misitu sura ya 323.

Nyingine ni Sheria ya uhamiaji sura ya 54, Sheria ya ajira na uhusiano kazini 366, Sheria ya mtoto sura ya 13, Sheria ya Mahakama za migogoro ya Ardhi sura 216, Sheria ya afya ya akili sura 98, Sheria ya Baraza la Kiswahili Tanzania sura ya 52, Sheria ya viapo sura ya 12.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles