26.6 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

Muswada kulinda viongozi wa mihimili ya dola wapita bungeni

Ramadhan Hassan -Dodoma

BUNGE limepitisha muswada wa marekebisho ya sheria mbalimbali wa mwaka 2020, kikiwemo kifungu cha viongozi wakuu wa mihimili ya dola kutoshtakiwa wakiwa madarakani.

Akiwasilisha muswada huo bungeni jana, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Profesa Adelardus Kilangi, alisema katika Sheria ya Masuala ya Rais, Sura ya 9, muswada unalenga kufanya marekebisho katika kifungu cha 6 ili mashauri dhidi ya Rais kwa mambo anayodaiwa kuyatenda yeye binafsi kama raia, yaliyoruhusiwa kufunguliwa dhidi yake kwa mujibu wa ibara ya 46(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yafunguliwe baada ya kutoka madarakani.

Alisema kifungu cha saba kinapendekezwa kurekebishwa ili mashauri yoyote dhidi ya Rais yafunguliwe dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

“Lengo la marekebisho haya ni kuwa na maudhui ya dhana ya kinga dhidi ya Rais ambayo ni kulinda hadhi ya Rais na nafasi yake,” alisema Profesa Kilangi.

Hata hivyo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilipendekeza kifungu hicho kifutwe na badala yake sheria iruhusu mtu aliyehusika katika uvunjifu wa Katiba au haki za kiraia kuwajibika katika mahakama.

Akiwasilisha maoni hayo, Msemaji Mkuu wa Kambi hiyo katika Wizara ya Sheria na Katiba, Salome Makamba, alisema kifungu cha 49 cha muswada kina mapendekezo ya marekebisho ya kifungu cha sita ili mashauri dhidi ya Rais kwa mambo anayodaiwa kuyatenda yeye binafsi kama raia na ambayo yameruhusiwa kufunguliwa dhidi yake kwa mujibu wa Ibara ya 46(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yafunguliwe baada ya kutoka madarakani.

“Ni dhahiri kwamba kifungu hiki kitakuwa kinakinzana na matakwa ya Katiba kwa kuwa kifungu cha 46 (2) kimeshaweka utaratibu wa namna ya kufanya. Kama kifungu hiki kitarekebishwa, kitakuwa kinakinzana na matakwa ya Ibara ya 46 (2) na kwa vyovyote vile sheria ya kawaida haitaweza kufanya kazi mbele ya Ibara ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Kifungu cha 7(1) cha Sheria ya Masuala ya Rais ambacho kinapendekezwa kurekebiswa ili mashauri yoyote dhidi ya Rais yafunguliwe dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

“Sasa haya makosa mbali ya yale yake binafsi yaliyoainishwa, ni makosa gani yatakayohitaji aunganishwe na AG ni yapi? Je, kama ni makosa yake binafsi kwa nini atumike Mwanasheria Mkuu wa Serikali? Kwa nini asimtumie mwanasheria wake binafsi?

“Sababu za mapendekezo haya ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ni kuongeza uwazi na uwajibikaji katika utumishi wa umma na usawa mbele ya sheria,” alisema Salome.

UMILIKI WA SILAHA

Vilevile, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Profesa Kilangi alisema katika Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Silaha na Risasi, Sura ya 223, muswada unakusudia kufanya marekebisho kwa kuongeza kifungu kipya cha 20 A ili kuweka katazo kwa wamiliki halali wa silaha na risasi kuhamisha silaha hizo kwa watu wasioruhusiwa kuzimiliki.

Alisema lengo la marekebisho hayo ni kuhakikisha kuwa kwa wakati wote silaha na risasi zinakuwa chini ya mmiliki halali.

KINGA KWA JAJI MKUU NA MAJAJI

Profesa Kilangi pia alisema katika Sheria ya Uendeshaji wa Mahakama, Sura ya 237, muswada unakusudia kufanya marekebisho kwa kuongeza kifungu kipya cha 65 A kwa lengo la kuweka masharti ya kinga dhidi ya mashtaka kwa Jaji Mkuu, majaji na maofisa wengine wa mahakama katika utekelezaji wa majukumu yao ya kimahakama.

MKURUGENZI WANYAMAPORI

Mwanasheria Mkuu wa Serikali alisema katika Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori, Sura ya 283, inapendekezwa kufanya marekebisho katika kifungu cha 116 ili kuondoa utaratibu wa Mkurugenzi wa Wanyamapori na maofisa wengine wa wanyamapori kutaifisha mifugo kupitia utaratibu wa kufililisha makosa na badala yake utaifishaji wa mifugo ufanywe kwa amri ya mahakama.

“Hatua hii itasaidia kuondoa malalamiko ya wafugaji na wananchi kwa ujumla dhidi ya watumishi husika kutokana na kutumia vibaya mamlaka hayo,” alisema Profesa Kilangi.

Aidha, alisema utaratibu unaopendekezwa utaleta uwiano na mfanano katika sheria hiyo, Sheria ya Hifadhi ya Taifa, Sura ya 282, Sheria ya Misitu, Sura ya 323 na Sheria ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Sura ya 284 katika kufililisha makosa.

KAMATI NA WAFUGAJI

Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria na Katiba, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mohammed Mchengerwa, alisema wamebaini na kutambua jitihada za Serikali katika kuweka mazingira mazuri na rafiki kisheria kuhusu haki za wafugaji nchini, ikiwemo kufuta mamlaka za kiutendaji zenye kuamua hatima ya mifugo ya wafugaji pasipo amri ya mahakama.

Mchengerwa alisema kwa kuwa yapo madhara mengi zaidi yanayoambatana na mifugo kuendelea kushikiliwa kwenye hifadhi pasipo uangalizi wa kutosha, hivyo basi, kamati inashauri Serikali kuwa elimu itolewe kwa jamii ya wafugaji wanaoishi karibu na hifadhi za taifa, kuhusu athari za mifugo kuingilia makazi ya wanyamapori.

Alisema kamati pia inashauri Serikali iandae mfumo thabiti na endelevu wa kisheria na kiutendaji utakaotoa majibu ya changamoto mbalimbali zenye kuathiri jamii ya wafugaji, wakulima na ustawi wa hifadhi za taifa kwa maendeleo endelevu ya taifa.

WABUNGE WATOFAUTIANA

Wakichangia mjadala huo, wabunge walitofautiana katika kifungu cha Rais kutoshtakiwa pindi anapokuwa madarakani.

Mbunge wa Viti Maalumu, Salome Makamba (Chadema) alisema haiwezekani kukatengenezwa kinga kwa watu ambao wanavunja sheria kwa makusudi, hivyo ni lazima washtakiwe ili haki iweze kutendeka.

“Mtashtakiwa tu, hii sheria haina nguvu, haiwezekani kukatengenezwa kinga kwa watu wanaofanya mambo makusudi, nasema hivi mtashitakiwa tu,” alisema Salome.

Mbunge wa Viti Maalumu, Latifa Chande (Chadema) alisema ni lazima wenye mamkala washtakiwe kwani binadamu wote ni sawa.

Hata hivyo, Mbunge wa Ulanga, Goodluck Mlinga (CCM) alisema rais ni lazima aheshimiwe huku akinukuu Qur’ani na Biblia kwamba wenye mamlaka wanatakiwa kuheshimiwa.

“Rais ni lazima aheshimiwe, haiwezekani aache nchi awe anaenda mahakamani,” alisema Mlinga.

Mbunge wa Viti Maalum, Asha Abdallah Juma (CCM) alisema anayepaswa kushtakiwa ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali na sio Rais pindi anapokuwa madarakani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles