28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Muswada bima ya afya kuwa lazima mbioni

Elizabeth Kilindi -Njombe

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, amesema hivi karibuni atapeleka bungeni muswada wa sheria ili bima ya afya iwe lazima kwa kila Mtanzania.

Kauli hiyo aliitoa jana mkoani hapa mara baada ya kufanya ziara ya siku moja katika Hospitali ya Rufaa Kibena.

Alisema Watanzania wajiandae ili kuweza kupata huduma bora za afya bila ya kikwazo. “Suluhisho ni kuwa na bima ya afya, lakini kwa watoa huduma za afya za Serikali, mtu akiwa na bima kama ni binafsi au Serikali anataka huduma bora kwa hiyo lazima mjipange madaktari, mtu mwenye bima asiende kwa mtu binafsi, mjipange kweli kweli,” alisema Ummy.

Aidha waziri huyo pia alitembelea bohari ya kuhifadhia madawa ya Hospitali ya Kibena ambako alisema kwa sasa upatikanaji wa dawa katika vituo vya afya ni mkubwa akitoa mfano kuwa Mkoa wa Njombe pekee upatikanaji wa dawa ni asilimia 96.

“Niseme kuna mbunge mmoja wa upinzani anasema hakuna dawa na mimi nataka kusema ni uongo, nipo hapa Njombe na hali ya upatikanaji wa dawa ni asilimia 96 na kigezo cha Shirika la Afya Duniani limebainisha dawa muhimu angalau aina 30, kwa hiyo haya sio maneno ya kwenye makaratasi au ya mitaani,” alisema Ummy.

Aliongeza; “Shirika la Afya Duniani wanatupima kwa aina 30 tu za dawa, lakini sisi tumeenda mbali mpaka aina 312. Tunafurahi hapa tupo Kibena dawa muhimu zinapatikana, baadhi ya watu wanafanya tu siasa.”

Kwa upande wa Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Zainabu Chaula, alisema kazi ya wizara ni kutengeneza sera, miongozo kutafuta fedha kwa wadau, lakini Serikali imejikita katika kuhakikisha yote yanafanyika kwa wakati.

“Sisi wenyewe hakuna haja ya kuwa walalamishi, uwezo wa kufanya tunao, yapo ndani ya uwezo wetu, lakini zaidi tuwahamasishe wagonjwa wetu wawe na bima za afya, mifumo ya bima ipo, sisi wenyewe hapa tupo kazini sio kwamba tuna hela, lakini utaratibu umetuweka watumishi wa Serikali wote tuna bima ambayo ni asilimia saba na asilimia 93 iko nje ya mfumo.

“Mwezi huu utaingia muswada kila mwananchi awe na bima, hii yenyewe peke yake itatuondolea mgogoro kwa sababu wale wenye bima wote wanaenda hospitali binafsi na wale ambao tunasema hawana uwezo ndo wanakuja kwenye hospitali zetu, kwa hiyo tunataka kufanya mabadiliko kila mwenye bima aje hapa, kila mtu awe na uhuru wa kuchagua,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles