Museveni: Bobi Wine adui wa Uganda

0
1375

RAIS wa UGANDA, Yoweri Museveni amemtaja mkosoaji wake mwanamuziki aliyegeuka kuwa mwanasiasa Bobi Wine, kama “adui wa mafanikio ya nchi hiyo”.

Rais Museveni ameyasema hayo katika mahojiano na BBC .

Museveni ambaye anataka kugombea muhula wa sita kama rais mwaka 2021 baada ya kutawala kwa miaka 33 alisema  Bobi alikwenda Marekani na kusema kwamba watu wasiende kuwekeza Uganda

Bobi Wine, ambaye ni kiongozi wa vuguvugu la ‘The People Power’, anamshutumu rais huyo kwa kuongoza kwa mfumo wa ukandamizaji.

 Museveni amekataa kumueleza mwandishi wa BBC kama  serikali yake ni ya ukandamizaji , lakini akasema anamshughulikia Bobi Wine kama adui.

”Unapoenda na kuwaambia wageni kwamba hawapaswi kuja na kuwekeza katika nchi yetu, inamaanisha umeanzisha vita dhidi ya mafanikio yetu. Kwa hiyo kwanini sasa unataka kurejea na kunufaika na mafanikio hayo?”.

“Hii huenda ndio moja ya sababu za kufutwa kwa matamasha ya muziki ya Bobi Wine, bado sijaongea na polisi kupata taarifa zaidi,” alisema.

Juhudi za Bobi Wine kuhamasisha umma dhidi ya Rais Museveni zimekuwa zikizimwa na maafisa wa usalama

Rais huyo wa Uganda anasema bado ataendelea kuwepo madarakani kwa miaka mingine zaidi kukamilisha kile ambacho yeye binafsi na wapiganaji wenzake walikipanga kukifanikisha katika nchi yao na Afrika.

”Nyumba yangu inanisubiri, lakini tuna masuala kama Uganda ya kushughulikia. Ni masuala hayo ambayo yanatufanya tufanye kile tunachotaka kukifanya kisiasa pamoja na wenzetu. Kama chama tawala (NRM) kitafikiria kuwa hakihitaji mchango wa wazee basi tutaondoka madarakani kwa furaha na kufanya mambo mengine,”  alisema Museveni katika mahojiano hayo yaliyofanyika mjini Kampala.

”Hatupo hapa kwa ajili ya maonyesho, hatuendi kwenye ukumbi wa michezo ya maigizo , sisi ni watu ambao tupo hapa kushughulikia masuala makubwa ya Uganda na Afrika,” alisistiza kiongozi huyo wa Uganda.

Kiongozi wa upinzani Dk. Kizza Besigye kama ilivyo kwa Bobi naye alikuwa akikabiliwa na nguvu ya maofisa wa usalama kila alipojaribu kuonyesha upinzani dhidi ya serikali ya Museveni.

Rais Yoweri Museveni ambaye amekuwa madarakani zaidi ya miongo mitatu amekuwa akikabiliwa na wito wa kumtaka ajiuzulu hasa kutoka kwa vijana na wapinzani wake .

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here