25.2 C
Dar es Salaam
Friday, August 12, 2022

Museveni alaumu kushambuliwa kwa Libya

London, Uingereza

RAIS Yoweri Museveni wa Uganda amesema haikupasa nchi za Afrika ziruhusu nchi za Magharibi ziishambulie kijeshi Libya na kupelekea kuuawa aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo, Kanali Muammar Gaddafi.

Museveni, ambaye yuko nchini Uingereza alikohudhuria mkutano wa uwekezaji kati ya Afrika na Uingereza, aliliambia Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) kuwa nchi za Afrika zilipaswa kuingilia kati nchini Libya na kwamba japokuwa zilijaribu kufanya hivyo kidiplomasia, lakini zingeweza pia kuingilia kijeshi.

Akizungumza kwa hasira, Museveni alisema laiti kama Afrika ingejiandaa vya kutosha, madola ya kigeni yasingeishambulia Libya na kumuua Gaddafi.

“Afrika ingeweza kuingilia kati na kutoa funzo kwa watu hao,” alisisitiza Museveni.

Aidha Museveni alisikitikia kifo cha Gaddafi, akikielezea kuwa ni matokeo ya Waafrika kushindwa kumlinda “mwana wao”.

Alifafanua kuwa Libya ni nchi ya Afrika ambayo ilishambuliwa na madola ya kigeni, hivyo nchi za bara hilo zilipaswa kuingilia kati. 

Katika mahojiano hayo na BBC, Museveni alisema Afrika haikupigana kuisaidia Libya kwa sababu shambulio dhidi ya nchi hiyo lilifanywa kwa kushtukiza.

Alifafanua kuwa hata yeye mwenyewe hakuweza kuamini kama kuna mtu anayeweza kuwa ‘mpumbavu’ kiasi cha kuishambulia nchi ya Kiafrika namna ile.

Aidha, Museveni alisema nchi za Afrika hazihitaji uingiliaji wa madola ya kigeni kutatua masuala yao ya ndani na akaongeza kuwa zinahitaji kuungana na kuongea “lugha moja” na kuweza kumshinda yeyote atakayejaribu kuwashambulia watu wao.

Alisema anaamini Afrika iliyoungana inao uwezo wa kuyashinda madola yoyote makubwa ya Magharibi yatakayojaribu kulivamia bara hilo, akikumbusha jinsi Afrika ilivyoweza kuwashinda na kuwatimua Wareno pamoja na makaburu waliokuwa wakisaidiwa na kuungwa mkono na madola hayo.

mwisho

Isabel dos Santos afunguliwa mashtaka ya ulaghai

LUANDA, ANGOLA

MWANAMKE tajiri zaidi Afrika, Isabel dos Santos amefunguliwa mashtaka ya ulaghai baada ya kutuhumiwa kulipora taifa hilo.

Mwanasheria Mkuu, Helder Pitta Groz alisema kwamba madai hayo yanahusiana na wakati alipokuwa mwenyekiti wa kampuni ya mafuta ya Sonangol.

Watu kadhaa pia wametuhumiwa pamoja na Isabel.

Groz alisema kwamba wataomba kibali cha kimataifa cha kuwakamata iwapo watagoma kujikabidhi wenyewe mbele ya mamlaka ya Angola.

“Isabel dos Santos anatuhumiwa kwa usimamizi na ufujaji wa fedha wakati alipokuwa mwenyekiti wa kampuni hiyo ya Sonangol, hivyo basi amefunguliwa mashtaka ya usimamizi mbaya wa ofisi, kutumia ushawishi wake na kughushi stakabadhi miongoni mwa uhalifu mwengine wa kiuchumi,” Groz aliuambia mkutano na wanahabari Jumatano jioni.

Alisema uchunguzi kuhusiana na usimamizi wake wa kipindi cha miezi 18 katika kampuni hiyo ya mafuta kuanzia Juni 2016, ulianzishwa baada ya mrithi wake, Carlos Satumino kuelezea mamlaka kuhusu uhamishaji wa fedha usio wa kawaida.

Stakabadhi zilivuja wiki hii zikidai kwamba Isabel, mwana wa aliyekuwa rais wa taifa hilo, Jose Eduardo dos Santos, alijipatia mali ya thamani ya dola bilioni 2.1 kwa kulipora taifa lake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,526FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles