30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Murathe ajiuzulu uongozi Jubilee apambane na Ruto

NAIROBI, KENYA

NAIBU Mwenyekiti wa Chama tawala cha Jubilee (JP), David Murathe amejiuzulu wadhifa wake huo, akisema hawezi kukaa meza moja na Naibu Rais William Ruto.

Akitoa tangazo hilo juzi, Murathe alisema hataendelea na umakamu mwenyekiti wa JP ikizingatiwa anapania kumzuia Ruto kuwania urais mwaka 2022.

Siku moja kabla ya kujiuzulu, alisema ataelekea Mahakama ya Juu kutaka ufafanuzi wa Katiba kuhusu hatma ya Dk. Ruto kuwania urais, pamoja na kumzuia.

“Sioni haja ya kusalia katika chama kama makamu mwenyekiti wakati huohuo kuwa katika baraza moja la Taifa la chama na mtu ambaye nitampeleka mahakamani kumzuia kuwania urais,” Murathe alisema.

Kwenye kikao na wanahabari mjini hapa, mbunge huyu wa zamani wa Gatanga alisema harakati za kumzuia naibu rais kuwania urais 2022 ni zake binafsi.

“Ninasimama kidete na matamshi yangu ambayo ni binafsi. Kuna watu tulio na mawazo sawa, lakini yasichukuliwe ya kurushiana cheche za matusi,” alisema.

Desemba 26, mwaka jana Murathe alizungumza na wakazi wa Kaunti ya Vihiga akisema jamii ya Mlima Kenya haijatia saini mkataba wowote kumuunga mkono Ruto kuwania urais mwaka 2022.

Alisema jamii hiyo haina deni lolote kwa naibu rais na kwamba iwapo Rais Uhuru Kenyatta ana ahadi yoyote ni suala lao binafsi; Kenyatta na Ruto.

Kuna madai kuwa Rais Kenyatta aliingia makubaliano ya kuongoza kwa muda wa 10 Ruto akiwa naibu wake kisha 2022 amuunge mkono kuwa rais.

Hata hivyo, Murathe alitupilia mbali suala hilo akitaka aliye na ushahidi aoneshe taifa mkataba huo.

Kauli ya Murathe kuhusu siasa za urithi za 2022 zimeibua hisia tofauti ndani ya Jubilee, wachangunuzi wa masuala ya kisiasa wakihoji iwapo ametumwa na Rais Kenyatta kutuma ujumbe.

Pamoja na Murathe kutoa kauli ya kujiuzulu, ripoti zinasema Ruto amemlalamikia Kenyatta, ambaye akamtaka mshirika wake huyo kujiuzulu ili kuepusha kukimega chama hicho.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles