27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

MUNA LOVE AWAGAWA MASHABIKI, MASTAA

CHRISTOPHER MSEKENA NA CLARA MATIMO


MWIGIZAJI Rose Nungu ‘Muna Love’ kwa mara nyingine ametengeneza vichwa vya habari kuanzia mitandaoni, runingani hadi kwenye kurasa za habari za burudani katika magazeti mbalimbali nchini.

Hiyo ni baada ya kuitisha mkutano na waandishi wa habari, Jumatano wiki hii nyumbani kwake, Mbezi Beach, jijini Dar es Salaam, ikiwa ni siku 11 tu tangu mwanaye Parick azikwe.

Katika mkutano huo, Muna ambaye kwa sasa ameokoka, alifafanua mambo kadhaa yaliyokuwa na utata likiwemo la baba halisi wa marehemu mwanaye na namna mchekeshaji Steven Mengele ‘Nyerere’ alivyopotosha watu kuhusiana na kukubaliana juu ya maziko ya mtoto wake.

Siku moja tu baada ya kusambaa kwa taarifa hizo, mashabiki mbalimbali na mastaa wenzake wameonekana kupingana kutokana na tukio hilo.

Baadhi ya mashabiki mitandaoni na mastaa, wamemnanga kwa kitendo chake cha kuitisha mkutano na waandishi wa habari, kabla ya 40 ya mwanaye, huku wengine wakimuunga mkono.

MUNA KIKAONI

Katika kikao hicho, Muna alisisitiza kuwa baba wa marehemu mwanaye hakuwa Peter Komu, kama ilivyoandikwa kwenye msalaba bali ni Casto Dickson na kwamba Peter alifunga naye ndoa akiwa na mimba ya Casto, jambo ambalo Peter mwenyewe alilijua na aliridhia.

“Nilikutana na Peter jijini Mbeya nikiwa nafanya kazi Safari Pool Table, tulikaa kwenye mahusiano kwa miezi miwili tukaingia kwenye ndoa, lakini kuna vitu nilivyokutana navyo kama binadamu nilishindwa, nikaamua kuendelea na maisha yangu.

“Wakati naingia kwenye mahusiano na Peter nilikuwa nina mimba ya Casto ya miezi miwili, Casto aliikana mimba hiyo ikiwa na wiki mbili. Baadaye alirudi wakati mtoto Patrick akiwa na miaka mitatu.

“Kwa sababu nilizaa nikiwa kwenye ndoa na Peter ndiye alisimamia hata ubatizo ndizo picha zilizosambaa, lakini hata yeye Peter anaujua ukweli kuhusu mtoto huyo,” amesema Muna.

KUHUSU STEVE NYERERE

Kuhusu Nyerere kusuluhisha mgogoro uliokuwepo kati yake na aliyekuwa mumewe Peter Komu na kuweka makubaliano na taratibu za mazishi kufanyika nyumbani kwa Komu Mwanananyama, amekanusha.

“Nilichoongea na Steve ni tofauti na nilichokiona kwenye mitandao, ukweli mimi sikumjibu chochote. Niliingia Tanzania nikiwa nimeishiwa nguvu kabisa. Nikiwa nyumbani walikuja wageni kutoka kwa kina Peter, wakanipa malalamiko, nikawaambia ninachohitaji ni kumzika mtoto wangu, sihitaji kuongea chochote.

“Wakasema wanaomba mtoto apelekwe Mwananyamala, tukaandikishiana mtoto apelekwe Mwananyamala. Ilibidi nikubali kwa kuwa sikutaka kumsumbua mwanangu. Kaka Steve kama alivyosema yeye mimi nimesema msiba ufanyike Mwananyamala, sikuongea naye hilo jambo kabisa, yaani msimamo wangu tangu siku ya kwanza ulikuwa vilevile nilivyosema,” alisema.

Baada ya kauli hiyo, aliwasikilizisha wanahabari voice note walizowasiliana na Nyerere kuhusiana na msiba wa mwanaye, akisisitiza kwamba suala la msiba kuwa Mwananyamala hakuongea naye kabisa jambo hilo.

AWAGAWA MASTAA

Kitendo cha Muna Love kufunguka mambo hayo, mastaa mbalimbali walitofautiana mitazamo huku wengine wakidai yupo sahihi na wengine wakisema hakukuwa na umuhimu wa kufanya hivyo.

Peter, aliyekuwa mume wa Muna ambaye yupo jijini Mwanza alikuwa wa kwanza kuzungumza na Swaggaz ambapo alisema ni mapema kuzungumzia suala hilo, kwa vile bado ana simanzi na kuondokewa na mwanaye.

“Nilipofika nyumbani kwangu   Mwananyamala  nilishangaa kukuta baadhi ya waandishi  wakinisubiri nje ya geti  langu hata waliponiuliza maswali kuhusiana na kauli za Muna niliwaambia siko tayari kuzungumza lolote, naomba nikuhakikishie ndugu mwandishi kwamba sitamjibu lolote mke wangu, nitaendelea kumlilia Mungu na kumwombea mwanangu maisha yote hapa duniani yeye (Muna) aendelee kuongea  akichoka atanyamaza,” alisema Peter Komu.

STEVE NYERERE

Steve Nyerere alisema: Sijutii kuratibu msiba wa Patrick kwa sababu mipango yote niliyopanga  kwa kushirikiana na baba mzazi Mr. Peter ilikwenda vile vile. Mtoto alikwenda kwao Mwananyamala na baadaye Leaders kama tulivyopanga, sasa kama Peter siyo baba mbona kwenye msalaba aliandika jina la Patrick Peter?

“Kwanza Muna inabidi ashitakiwe kuwasiliana na jasusi wa nchi kama Mange Kimambi, inawezekana hata siri za nchi anazitoa yeye.”

NAY WA MITEGO

Msanii wa muziki wa Bongo Fleva, Emmanuel Elibariki ‘Ney wa Mitego’, yeye anasema ni haki ya Muna kuzungumza anachojisikia akiwa kama mama, hakuna mtu yeyote anayeweza kumzuia na wasanii walioonekana kumkosoa wanakosea sana.

MC PILIPILI

Mchekeshaji maarufu Bongo, Emmanuel Mathias maarufu MC Pilipili ambaye alikuwa mshereheshaji wa msiba wa mtoto Patrick, anasema kwake ni sahihi kwani amejibu maswali ya watu wengi kwenye jamii kuhusu baba mzazi.

“Muna amefanya kitu kizuri, ni haki yake kusema ukweli sababu amejibu maswali ya watu wengi kwenye jamii. Yule mtoto alikuwa ni wa jamii, na jamii inapopata kusikia kitu haina budi kupewa majibu kama ambayo Muna ameyatoa,” anasema.

 SHILOLE

Mwigizaji Bongo Muvi na msanii wa Bongo Fleva, Zuwena Mohamed ‘Shilole’ amelaani vikali kitendo cha Muna kuzungumza na waandishi wa habari mapema baada ya kumzika mwanaye, lakini pia kueleza mambo ya ndani ambayo ni siri yake na familia.

“Kiukweli nimekasirishwa sana, nimechukizwa sana na kitendo cha Muna kuita waandishi wa habari ikiwa bado ni mapema sana. Mwanamke ambaye umezaa mtoto, umehangaika naye, mtoto amefariki, aliumwa sana, Mungu akamchukua kwa mapenzi yake, unaweza kuwaita waandishi wa habari hata 40 haijafika?

“Kwa ninavyojua mimi, kuondokewa na mtoto kunauma sana. Naongea kama mama, juzi tumemzika mtoto, halafu leo unaita waandishi wa habari. Ili iweje? Hata kama una matatizo na Peter kwanini usifiche? Kwanini usifiche aibu ya wanawake wenzako? Im speechless.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles