Mume wa Zamaradi kufikishwa kizimbani kwa kutishia kuua

0
931

ELIZABETH HOMBO-DAR ES SALAAM

KAMANDA wa Polisi Kinondoni, Mussa Taibu, amesema wanamshikilia Shaban Hamis Said ambaye ni mume wa mtangazaji maarufu nchini, Zamaradi Mketema, kwa kosa la kutishia kuua na anatarajiwa kufikishwa mahakamani kesho.

Kabla ya Kamanda Taibu kuthibitisha kumshikilia Shaban, MTANZANIA Jumapili lilidokezwa kuwa alikamatwa juzi baada ya swala ya Ijumaa na kupelekwa moja kwa moja kituo cha polisi ambako anashikiliwa hadi sasa.

Hatua ya kukamatwa Shaban, imekuja baada ya juzi, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro kuagiza kukamatwa akituhumiwa kumtishia dereva mwenzake kwa bastola.

Alipoulizwa na MTANZANIA Jumapili jana, endapo wanamshikilia mume huyo wa Zamaradi, Kamanda Taibu alisema ni kweli wanamshikilia na kwamba atafikishwa mahakamani kesho.

 “Niko kwenye kikao na sijui tunatoka saa ngapi, lakini kwa ufupi ni kweli tunamshikilia tangu jana (juzi) na tutampeleka mahakamani Jumatatu,” alisema Kamanda Taibu.

Kuhusu sababu za kumshikilia, Kamanda Taibu alikiri kuwa wanamshikilia kwa kumtishia kumuua kwa bastola dereva wa lori, Venance John, Oktoba 30 mwaka huu maeneo ya Mabwepande, Dar es Salaam.

Jioni ya Alhamisi ya wiki hii, ilisambaa video inayomwonyesha Shaban aliyekuwa na gari dogo lenye rangi ya bluu, akitishia kumpiga risasi dereva mwenzake aliyekuwa akiendesha gari kubwa.

Juzi, IGP Sirro aliwaambia waandishi wa habari kuwa watu hupewa silaha kwa masharti maalumu na kwamba hawakuwapa ili wawatishie Watanzania.

Mbali na hilo, IGP Sirro alisema kuwa licha ya kutofahamu sababu ya ugomvi uliosababisha kijana huyo kutoa silaha, lakini suala la kujiuliza ni kama kulikuwa na ulazima kumtishia mwenzake silaha.

“Tukibaini umetishia Watanzania kama alivyofanya yule kijana, hatujui ugomvi ulikuwa ni nini, lakini je, kama ni kweli yale yaliyokuwa yanaelezwa kulikuwa na ulazima wa kutoa silaha kumtishia mwenzake?

 “Kimsingi mtu ukipewa silaha hakikisha unafuata yale masharti, usipofuata masharti la kwanza tutakunyang’anya silaha, lakini la pili tutakupeleka mahakamani na la tatu tutamwomba Mungu tukufunge ili ukirudi nyumbani kwa mke wako au kwa mume wako uwe na adabu ya kutunza vitu vyako,” alisema IGP Sirro.

Katika video hiyo, dereva wa gari kubwa alianza kusikika akimwambia mume huyo wa Zamaradi kuwa; “umesema unatoa bunduki itoe hiyo bunduki.”

Wakati mzozo huo ukiendelea, dereva wa gari dogo ambaye ndiye mume huyo wa Zamaradi, aliyekuwa amevaa shati jeupe, alielekea katika gari lake na kutoka na bastola.

Pamoja na kutoka na bastola, dereva wa gari kubwa hakuonyesha kutishika na kitendo hicho na kumwambia kuwa kama anataka kumshambulia kwa bastola haogopi kwa sababu alizaliwa ni lazima atakufa.

“Mimi kufa nitakufa na wewe utakufa, huna lolote, nakwambia kweli huna lolote, toa hiyo bunduki, mwache aniue,” alisikika akisema dereva wa gari kubwa.

Licha ya Shaban kumwamuru akae chini huku akitoa maneno makali, bado dereva huyo alikataa huku akisisitia kuwa kama anataka amuue.

Pia Shaban alionekana akimwelekezea kichwani mwenzake bastola hiyo na kumweleza kuwa atampasua.

Juzi na jana, gazeti hili lilimtafuta kwa njia ya simu Zamaradi ili aweze kuzungumzia kuhusu mume wake kuonekana katika video hiyo, lakini simu yake iliita bila kupokewa na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maandishi kwa njia ya mtandao wa WhatsApp licha ya kusomwa haukujibiwa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here