26.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

Mume wa Zamaradi afikishwa kortini kwa kosa la kutishia kuua kwa kutumia nguvu

ERICK MUGISHA-DAR ES SALAAM

MFANYABIASHARA Shabani Hamisi (33), mkazi wa Mabwepande, Dar es Salaam, amepandishwa kizimbani Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni kwa kosa la kutishia kuua kwa kutumia nguvu.

Hamisi ambaye ni mume wa mtangazaji maarufu nchini. Zamaradi Mketema, alikamatwa baada ya kusambaa kwa video yake katika mitandao ya kijamii ikimwonyesha akizozana na dereva wa daladala, huku akimtolea bastola akitishia kutaka kumuua.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mkunde Mshanga, jana alimsomea Hamisi hati ya mashtaka mbele ya Hakimu Frank Mushi, ambapo alidai Oktoba 30 mwaka huu, majira ya mchana akiwa eneo la Mabwepande wilayani Kinondoni, Dar es Salaam akiwa mmiliki wa bastola yenye namba za usajili 102969 aina ya Geleta kwa makusudi alimtishia Venance John.

Hata hivyo mshtakiwa huyo alikana kutenda kosa hilo na Wakili Mshanga alidai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kuomba mahakama tarehe nyingine kwa kutajwa.

“Upelelezi wa shauri hilo haujakamilika na tunaomba mahakama ipange tarehe nyingine kwa kutajwa na kosa linalomkabili mshtakiwa linadhaminika, tunaomba mahakama kumpatia dhamana mshtakiwa,” alidai Mshanga.

Hakimu Mushi alisema dhamana kwa mshtakiwa ipo wazi kwa masharti ya kuwa na wadhamini wawili waaminifu, wenye barua za utambulisho kutoka Serikali za mtaa au kutoka kwa waajiri wao, nakala ya kitambulisho cha taifa au kitambulisho cha kupiga kura na kusaini bondi ya Sh 2,000,000 kwa kila mdhamini.

Mshtakiwa alitimiza masharti ya dhamana na kesi itakuja kwa kutajwa tena Desemba 13.

Mwisho.

Vijana CCM wamvaa Zitto Kabwe

Na mwandishi wetu –dar es salaam

UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa, umemvaa Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe  kwa kumtaka aache kutumiwa na waliodai kuwa mabeberu wa kisiasa.

Akizungumza Dar es Salaam jana wakati akiwapongeza vijana waliochukua fomu na kujitosa kuwania nafasi za uenyekiti na ujumbe wa Serikali za mitaa katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Novemba 24, Kaimu Mkuu wa Idara ya Uhamasishaji na Chipukizi UVCCM Taifa, Leonard Singo, alirusha kombora kwa Zitto na kudai amedandia hoja kuhusu uteuzi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG).

Singo alisema kuwa UVCCM inampongeza Rais Dk. John Magufuli  kwa uteuzi wa CAG mpya kwani hakusema yoyote aliyokosea kwa mamlaka aliyonayo kwa mujibu wa sheria.

“Zito Kabwe anachofanya UVCCM tunakijua pamoja na kundi lake, aache kutumika na mabeberu wa kisiasa, tunamuomba akae kimya,” alisema Singo.

Alimtaka Mbunge huyo wa Kigoma Mjini, akae kimya na asipotoshe Watanzania wakati Serikali ya awamu ya tano ya Rais Magufuli inafanya kazi.

Katika taarifa yao kwa vyombo vya habari muda mfupi baada ya uteuzi wa Kichere jana, ACT Wazalendo ilisema kwa mara nyingine Katiba ya nchi imevunjwa ilhali aliyepo bado anapaswa kuendelea kuwa madarakani.

Taarifa hiyo iliyotolewa na Mratibu Mawasiliano ACT Wazalendo Taifa, Mbarala Maharagande, ilisema kuwa Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe ambaye pia amewahi kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (POAC) kwa miaka nane (2007-2015 ), ameeleza kusikitishwa kwake na hatua ya kuondolewa kwa Profesa Assad.

Alisema kwa mujibu wa sheria ya ukaguzi ya taifa ya mwaka 2008, muda wa kukaa madarakani wa CAG ni vipindi viwili vya miaka mitano mitano, isipokuwa tu kama ametimiza umri wa miaka 65 na kama hakuna masuala ya nidhamu kwa mujibu wa Katiba, ni lazima ahudumu kwa mihula miwili, lakini huyo amehudumu kwa muhula mmoja tu na kwa sasa ana miaka 58.

Akizungumzia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Singo aliwapongeza vijana wa UVCCM pamoja na chama kwa kuwamini pamoja na Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ally ambaye amekuwa mstari wa mbele kupinga rushwa, lakini pia amekuwa akiwaamini vijana katika nafasi mbalimbali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles