MUME AUA MKE KISA KACHUMBARI

0
667

Kachumbari

Na Kadama Malunde -Shinyanga

MKAZI wa Mtaa wa Mageuzi, Manispaa ya Shinyanga, Stella Ibrahim (39), anadaiwa kuuawa kwa kupigwa na kitu kizito kichwani na mume wake, Ibrahim Daniel kwa kile kilichoelezwa  kuwa alipewa kachumbari iliyochacha.

Tukio hilo limetokea juzi usiku, baada ya Daniel kumshushia kipigo mkewe akidai kuwa alimpa kachumbari ambayo haikuhifadhiwa vizuri na mboga nyingine aliyodai haina kiwango.

Mashuhuda wa tukio hilo, walidai kuwa Daniel alifika nyumbani akiwa amelewa, kisha kuulizia  kachumbari ambayo alikula jana, ndipo mtoto wake, Elizabeth Ibrahim (13) akamwonesha kachumbari  ambayo inadaiwa tayari ilikuwa imechacha.

Walisema hakufurahia kuona kachumbari hiyo imeharibika, ndipo alipoanza kuuliza kwanini haikuhifadhiwa vizuri.

Akisimulia mkasa huo, mtoto wa marehemu, Daniel Ibrahim (12) alisema baba yeke alifika nyumbani saa moja usiku, alimkuta yeye akiwa na mdogo wake, Elizabeth aliyemuhoji kwanini kachumbari imeharibika, lakini hakupata jibu.

“Baada ya kuingia ndani, baba alimuuliza Elizabeth kachumbari aliyoiacha (Januari 16, mwaka huu) iko wapi, akaoneshwa. Baada ya kuiangalia aliiona imechacha, alitoka nje na kuchukua fimbo ambayo huwa anaiweka juu ya nyumba na kutaka kuanza kumpiga. Kabla ya kuanza kumpiga Elizabeth alikimbia.

“Baada ya Elizabeth kukimbia, mama ambaye alikuwa kazini alifika nyumbani, akamkuta baba akifoka, akauliza kuna nini, baba akasema kwanini hakupika mboga yenye kiwango na kwanini ulipikwa ugali mwingine wakati  kulikuwa na ugali uliobaki mchana,” alieleza mtoto huyo.

Alisema kutokana na maswali hayo, mama yake alimjibu kwa hasira kwanini hakuacha fedha nyumbani za kununulia mboga yenye kiwango anachotaka.

“Lakini majibu hayo yalionekana kumkera baba na kuanza kumpiga mama kwa kikombe na mateke, akaanguka, ninakimbia kuwataarifu majirani ambao walikuja na kukuta mama yuko hoi,” alieleza Daniel.

Mmoja wa majirani waliofika eneo la tukio, Leticia Mashala, alisema walipofika walikuta mlango umefungwa wakaanza kumgongea ili afungue.

“Tulipomgongea alikataa kufungua mlango na kusema ana kazi kidogo anaifanya tusubiri, lakini tulichungulia dirishani tukamwona anampuliza puani na masikioni, huku akimmwagia maji ili azinduke, baada ya kuona hazinduki alifungua mlango,” alisema Leticia.

Naye Shangazi wa marehemu, Getruda Vitalis, alisema wanandoa hao wamekuwa wakigombana mara kwa mara na wamewahi kusuluhishwa hadi kanisani walikofungia ndoa yao.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Mageuzi, Emmanuel Joshua, alisema chanzo cha mauaji hayo ni kachumbari iliyochacha iliyokuwa imetunzwa vibaya na mtoto waliokuwa wakimlea,  Elizabeth.

“Baada ya baba anayedaiwa alikuwa amelewa kudai kachumbari yake, mama aliingilia kati, akajikuta anaambulia kipigo… vipimo vya daktari vinaonyesha alipigwa na kitu kizito kwenye utosi, kichwa kikavimba na damu kavujia ndani kwa wingi,” alisema.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Elias Mwita, alisema mtuhumiwa Ibrahim Daniel anashikiliwa na jeshi hilo na baada ya marehemu kuchunguzwa alionekana kuwa na jeraha katikati ya kichwa chake.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here