24.5 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

MUME ALIVYOMWAGIA MKEWE MAJI YA MOTO KISA MAHINDI

Na VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM


“NAIKUMBUKA vema siku aliyonifuata na kuniambia ananipenda na yupo tayari kuishi na mimi maisha yake yote, sikusita kumkubalia kwani nilihisi damu zetu zilikuwa zimeendana, hivyo nilimkubalia.”

Ndivyo alivyoanza kujieleza, Neema Mwita mkazi wa Mara alipozungumza na MTANZANIA wodi namba 24, jengo la Sewahaji lililopo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

Anasimulia; “alilipa mahari iliyotakiwa nyumbani kwetu na tukapewa baraka na wazee, tukafunga ndoa kanisani, nakumbuka siku ile jinsi tulivyokuwa tukitembea kwa unyenyekevu kuelekea madhabahuni.

“Sikuwahi kufikiria kwamba ipo siku atabadilika tabia na kunisababishia matatizo makubwa kwenye maisha yangu, licha ya kumzalia watoto watatu.”

 

Nini kilitokea

“Siku moja nikiwa na mimba ya miezi minne, nilihisi njaa, nikaingia shambani kwetu nikachuma mahindi mawili ili nile na wanangu, nikiwa nimekalia kigoda jikoni, mume wangu akaja kuhoji kwanini nilichuma mahindi shambani… yalikuwa mawili tu.

“Akaniambia ngoja nije nikusaidie kuyachoma, akatoka nje nikajua kweli anakuja kunisaidia lakini aliporudi alianza kunipiga, akanidondosha chini kasha akachukua maji jikoni na kunimwagia yaliniunguza kifuani, akanifungia ndani,” anasimulia.

Anasema baada ya muda mtoto wake mmoja aliingia katika chumba hicho kwa siri na kumpelekea uji ili angalau ale.

“Baadae wakaja wasamaria wema wakanisaidia nikaondoka kwenda Musoma, lakini kadri nilivyokaa nyama ya kifua na shingo zilikuwa zikiendelea kushikana, siku moja alikuja Joyce Kiria akanionea huruma jinsi nilivyoungua,” anasema.

Anasema Kiria alimsaidia kumnunulia simu na kumuunganisha na watu ambao waliweza kumsaidia fedha na hivyo kuanza matibabu.

Neema anasema hawezi kusahau tukio hilo lilitokea miaka miwili iliyopita kwani limemsababishia jeraha kubwa katika maisha yake.

“Nilikuwa naumia mno, nikijikuna navimba, ilifika wakati sauti ilikuwa inakwama kutoka, watu waliendelea kuwasiliana na mimi, ndipo Rais John Magufuli alipopata taarifa zangu na kuamua kunisaidia,” anasema.

Ndugu walimtenga

“Tangu wakati huo hadi leo sijui huyo baba alikimbilia wapi na hajarudi kijijini hadi leo, baadhi ya ndugu zangu waliogopa kunisaidia na hata kunichukua nikae nao.

“Walihofu kwamba huenda siku moja angerudi hivyo asingenikuta ingeleta matatizo mengine, kwani alikuwa amelipa mahari nyumbani kwetu na kule (kijijini) mahari inaheshimiwa,” anasema.

Safari ya matibabu ilivyokuwa

Ibrahim Mkoma ni miongoni mwa madaktari bingwa wa Muhimbili aliyehusika tangu mwanzo kumfanyia upasuaji mama huyo.

“Tulimpokea hapa Muhimbili Julai, mwaka 2015 akitokea mkoani Mara ambapo alipewa rufaa. Sehemu ya kidevu na mkono wake wa kushoto vilikuwa vimeungana na sehemu ya shingo, alikuwa hawezi hata kugeuka kutoka upande mmoja hadi mwingine,” anasema.

Anasema Julai 21, mwaka huo walimfanyia upasuaji wa awamu ya kwanza ambapo walizitenganisha sehemu hizo.

Anabainisha kuwa kuna baadhi ya sehemu zilikuwa ngumu kushikana hasa kwenye shingo na kidevu na kwenye kwapa lake la kushoto hivyo Agosti, mwaka huo huo walimrudisha tena chumba cha upasuaji na kuchukua ngozi kutoka sehemu za mapaja yake na kujaza katika maeneo ambayo hayakushikana vizuri.

Anasema baada ya hapo aliweza kugeuza shingo kutoka upande mmoja hadi mwingine na kunyanyua angalau kidogo mkono wake wa kushoto.

Daktari huyo anasema kuwa mwanzoni mwa Septemba, mwaka huo walimruhusu kurejea nyumbani kwake.

Anasema ilipofika Novemba, mwaka huo walipokea ugeni wa madaktari bingwa wa upasuaji wanawake kutoka nchini Ujerumani na Uswizi ambao

walikuja nchini kwa ajili ya kuwafanyia upasuaji wanawake waliokuwa wameathirika na majanga mbalimbali hasa ya kuungua moto.

“Neema tulimjumuisha katika kambi hiyo na Desemba, tulimfanyia tena upasuaji kwa kushirikiana na madaktari hao. Awamu hii tulichukua ngozi kutoka sehemu yake ya tumboni tukawa tumebandika tena kwenye shingo ili iwe rahisi kuigeuza,” anasema.

Anasema walimlaza wodini na kuendelea kumpatia matibabu hatimaye afya yake ikaanza kuimarika.

“Februari, mwaka jana tulimruhusu kurejea nyumbani kwake, lakini wagonjwa kama hawa walioathirika na majanga makubwa kama neema wanahitaji msaada wa karibu wa jamii, msaada wa kifedha, na hata saikolojia ili afya yao iendelee kuimarika,” anasema.

Daktari huyo anasema mapema mwaka huu, Neema alianza kulalamika tena kusikia maumivu katika baadhi ya sehemu za mwili wake ikiwamo mkono na kwenye kwapa la kulia.

“Ilibidi arudi hospitalini kule Mara anapoishi, walipompokea lakini walishindwa kumuhudumia vizuri ikabidi wampe rufaa kuja huku Muhimbili,” anasema.

Anasema Februari, mwaka huu Rais Magufuli alisikia habari za mama huyo na akawa ameguswa na tatizo lake hivyo kuamua kumsaidia.

“Kwa kweli Rais Magufuli amekuwa msaada mkubwa mno, tumeendelea kumuhudumia na awamu hii tulimkuta na tatizo ambalo kitaalamu tunaliita ‘post traumatic stress disorder’,” anasema.

Anafafanua kwamba ni tatizo la kiafya ambalo linatokana na mtu kuathiriwa na kitu chochote kitakachomsababishia maumivu makali ya kisaikolojia, kimwili na hata kiroho.

“Sasa Neema aliathiriwa tena na mtu wake wa karibu, ule moto umemuathiri sehemu kubwa ya mwili wake, katika hali ya namna hii, mgonjwa anakuwa na malalamiko ambayo wakati mwingine huwa hayatokani na sehemu zenye majeraha moja kwa moja bali ni tatizo la kisaikolojia,” anasema.

Anasema baada ya kubaini hilo, waliamua kushirikiana na wataalamu wenzao wa saikolojia, mifupa na mazoezi ya viungo ambapo kwa pamoja waliendelea kumfanyia matibabu mama huyo.

Atabaki mlemavu

Anasema kwa kuwa alijeruhiwa vibaya na ule moto kuna baadhi ya sehemu za mwili wake zitabaki kuwa na ulemavu wa kudumu.

“Sehemu hizo ziliathiriwa mno na ule moto, kwa mfano kwenye mkono wake wa kulia ulipenya hadi kwenye mifupa na hivyo umemsababishia ulemavu.

“Kwa sasa bado hatuna utaalamu kuweza kurekebisha sehemu zilizoathirika namna hiyo, lakini tunashukuru tumeweza kumrejeshea angalau hali yake, anaweza sasa kusaidia familia yake kama mama,” anasema.

 

Tumaini larejea

Neema anasema anamshukuru Rais Magufuli na watu wote waliojitolea kumsaidia tangu walipopata taarifa za tatizo lake.

“Nilikuwa nimekata tamaa ya maisha, nilitamani nimeze dawa nijiue, niliambiwa nisubiri nife lakini leo hii nimepona, natamani nikitoka hapa nikaishi Mwanza ili nifanye ujasiriamali, pale kuna ziwa naweza kuuza samaki nikapata fedha,” anasema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles