20.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, September 28, 2022

MULEBA YAUNGANISHWA RASMI GRIDI YA TAIFA

                                                               |Mwandishi Wetu, MulebaWilaya ya Muleba mkoani Kagera, leo imeunganishwa rasmi na umeme wa gridi ya Taifa hatua itakayoifanya wilaya hiyo kuwa na umeme wa uhakika.

Akizungumza katika uzinduzi wa umeme huo leo Julai 29, uliofanyika katika Kijiji cha Nyamagojo Wilayani Muleba, Waziri wa Nishati, Dk. Kalemani, amesema Serikali imejipanga kuhakikisha kila Mtanzania hasa wa maeneo ya vijijini wanapata umeme kwenye nyumba zao.

Amesema katika utekelezaji wa mradi huo wa ujenzi wa KV 33 wa umeme wa gridi ya Taifa kutoka Wilayani Chato, Rais  John Magufuli, aliridhia na kutoa Sh milioni 778 ili kukamilisha kazi hiyo.

“Kuzinduliwa kwa umeme huu wa gridi ya Taifa sasa kuzifanya Wilaya za Muleba, Biharamulo na Ngara sasa kuwa na umeme wa uhakika wa hapa nchini kwetu. Tena umeme huu ni salama zaidi maana awali tulikuwa tunategemea umeme kutoka kwa wenzetu wa Uganda jambo ambalo hata wakizima kule hatuna namna ya kuuliza.

“Kati ya vijiji zaidi ya 600 vya Kagera hadi sasa vijiji zaidi ya 400 vina umeme lakini kuna vijiji zaidi ya 100 navyo wakandarasi wako kazini wanaendelea na kazi.

“Hivyo ni vema wananchi wakati muda huu wakandarasi wakiendelea na kazi ya kuunganisha vijiji umeme mkalipia Sh 27,000 ili muweze kuunganishiwa huduma ya umeme ndani ya siku saba,” amesema Dk. Kalemani.

Pamoja na mambo mengine, amewataka mameneja wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), nchi nzima kuhakikisha wanafanya kazi hiyo ikiwamo kwenda kukagua miradi na kuongeza kuwa asiyeweza kwenda na kasi hiyo atamuondoa ili apishe waliokuwa tayari kufanya kazi.

Awali akiwasilisha taarifa kwa Waziri kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Richard Muyango, amesema hatua ya kuunganisha mkoa huo kwenye gridi ya Taifa kutaufanya mkoa huo kuwa na umeme wa uhakika ambao ndiyo suluhisho la uhakika kwa uchumi wa kati na wa viwanda katika nchi yetu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
202,097FollowersFollow
554,000SubscribersSubscribe

Latest Articles