29.7 C
Dar es Salaam
Monday, October 2, 2023

Contact us: [email protected]

Muhimbili yahitaji ukarabati mkubwa

MUHIMBILINa Veronica Romwald, Dar es Salaam

UCHAKAVU wa miundombinu ya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ikiwamo ya majitaka, vifaa na majengo ni changamoto zinazohitaji kufanyiwa marekebisho makubwa.

Kauli hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki na Kaimu Mkurugenzi wa MNH, Profesa Lawrence Museru, alipozungumza kwenye hafla ya kuwatunuku vyeti wafanyakazi bora 53 kwa mwaka 2015/16.

“Hospitali hii ilijengwa miaka 60 iliyopita, kwa mara ya mwisho ukarabati ulifanywa miaka 20 iliyopita, leo hii majengo mengi yamechakaa na miundombinu ya majitaka imezidiwa na idadi ya watu, wakati wa mvua huwa ni changamoto kubwa.

“Ili kuendesha shughuli za kila siku za kutoa huduma, zinahitajika Sh. milioni 220 kwa ajili ya kulipia bili ya umeme Tanesco kila mwezi, Sh milioni 100 za bili ya maji Dawasco na Sh milioni 20 za kodi ya majengo,” alisema.

Alisema licha ya fedha kukusanywa kutoka kwa wagonjwa waliokuwa wakihudumiwa, baadhi zilikuwa haziingiziwi katika mfuko wa hospitali.

“Kulikuwa na upotevu wa mapato, mahitaji halisi ni zaidi ya Sh bilioni nne, zilizokuwa zikiingizwa kwenye mfuko ni takribani Sh bilioni mbili pekee, ndio maana ikawa inakabiliwa na madeni mengi hadi ya stahiki za wafanyakazi wake kwa sababu ilikuwa ikijiendesha kwa hasara,” alisema.

Alisema tangu waboreshe mifumo ya ukusanyaji wa mapato, wameweza kukusanya ya Sh bilioni 4.8 kufikia Mei mwaka huu kutoka Sh bilioni 2.4 Novemba, mwaka jana.

“Kulikuwa na pengo la Sh bilioni 2.1, kwa makusanyo hayo tumeweza kulipa madeni mbalimbali ikiwamo stahiki za wafanyakazi. Hivyo, tumeona tuwape motisho wafanyakazi hawa watatu  kati ya 3200 ili kuwapa ari wao na wenzao ya kufanya kazi kwa bidii,” alisema.

Alisema pamoja na hayo, wamejipanga kuboresha huduma zaidi kwa kuongeza vyumba vya upasuaji kutoka 13 vilivyopo sasa hadi 19 pamoja na wodi moja ya kulaza wagonjwa wa kulipia.

Alisema pia wataanza kutoa huduma ya kupandikiza figo na sikio ifikapo Januari  mwakani, ili kupunguza idadi ya watu wanaokwenda nje ya nchi kufuata huduma hizo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
575,000SubscribersSubscribe

Latest Articles