Na Mwandishi wetu Dar es Salaam
UONGOZI wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), umesema unaangalia jinsi ya kuboresha mfumo wa kliniki wagonjwa wahudumiwe kwa wakati wajnapofika hospitalini hapo.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili, Profesa Lawrence Museru, alipozungumza na madaktari bingwa kuhusu namna bora kuboresha huduma za matibabu katika hospitali hiyo.
Hospitali hiyo inahudumia wagonjwa wa nje 1,500 kwa siku huku wengine kati ya 1,200 hadi 1,300 wakiwa wamelazwa wodini wakati wote.
Profesa Museru alisema hatua wanazotaka kuchukua zitaboresha huduma katika kliniki za hospitali hiyo na kuondoa msongamano wakati wagonjwa wakisubiri kuona madaktari.
“Wakuu wa idara kupitia kwa madaktari mtuletee mapendekezo ambayo tutaangalia jinsi ya kujenga mazingira bora ambayo wagonjwa watatumia muda mfupi kumuona daktari.
“Tunataka mgonjwa asikae muda mrefu kwenye foleni,”alisema Profesa Museru.
Alisema uongozi wa hospitali hiyo chini ya bodi ya wadhamini, utaendelea kuboresha mazingira ya kufanyia kazi na kutoa huduma bora kwa wananchi.
“Naomba tuendelee kutumia vizuri miundombinu iliyopo kuongeza tija na wananchi wametuamini ndiyo maana wengi wamekuwa na matumaini makubwa na huduma tunazotoa,” alisema.
Akizungumzia upatikanaji wa dawa katika hospitali hiyo, alisema licha ya dawa kupatikana kwa zaidi ya asilimia 95, hospitali inaendelea kuimarisha utoaji wa dawa kwa wagonjwa kuhakikisha kila mgonjwa anayetibiwa anapata dawa kwa wakati.
Katika mkutano huo, madaktari walijadili njia za kuimarisha utoaji wa huduma bora za matibabu kwa wagonjwa mbalimbali na kukubaliana kufanya kazi kwa juhudi kufikia malengo yaliowekwa na hospitali hiyo, ya kutoa huduma bora za ubingwa wa juu nchini. Hospitali ya Taifa Muhimbili ina wafanyakazi 2,705, kati yao madaktari ni 328, ambako madaktari bingwa ni 186 na 142 ni madaktari wa kawaida. Hospitali ina wauguzi 946 na waliobaki ni wafanyakazi wa kada nyingine