MUHAS, Ufaransa kushirikiana kwenye afya, ajira, kubadilishana wanafunzi

0
799

Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Chuo Kikuu cha Afya na Tiba Shirikishi cha Muhimbili (MUHAS) kimesaini makubaliano ya ushirikiano na Chuo Kikuu cha Bordeaux cha nchini Ufaransa katika nyanja za afya.

Balozi wa Ufaransa Frédéric Clavier na Makamu Mkuu wa MUHAS Profesa Andrew Barnabas wamesaini makubaliano hayo jijini Dar es Salaam hivi karibuni wakati wa kongamano la wanafunzi wa Vyuo Vikuu vya Tanzania na Ufaransa.

Kongamano hilo lilishirikisha wanafunzi zaidi ya 900 waliojadiliana masuala mbalimbali ikiwamo namna ya kupata ajira katika kampuni 40 za uwekezaji zilizopo nchini.

Akizungumza baada ya kutia saini, Profesa Barnabas alisema ushirikiano huo utahusu afya ya mazingira na afya sehemu ya kazi.

“Ushirikiano wetu utahusu zaidi afya ya mazingira kwa binaadamu kwenye muingiliano wa watu na mimea, tutaangalia hasa katika mimea na matumizi ya dawa za viwandani zinavyoathiri afya za binadamu.

“Hawa wenzetu wa Bordeuaux wana uzoefu wa muda mrefu pia ni chuo kikubwa, sisi tuna wanafunzi 4,400 kwa mwaka wao wana wanafunzi 66,000 wa fani tofauti kwa wakati mmoja.

“Makubaliano haya yatasaidia sana kwenye tafiti zetu na kukuza kazi za kitafiti lakini pia kusaidia kwenye kutunga sera katika kusaidia taifa kukinga afya za binadamu na maradhi tunayoweza kudhibiti,” amesema Profesa Barnabas.

Makubaliano hayo yanaifanya Ufaransa kufungua milango kwa Watanzania wengi zaidi kusoma nchini kwao kwa kuongeza nafasi za ufadhili kutoka 30 hadi 50 kwa mwaka.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here