30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

MUGABE: SITAMPIGIA KURA MNANGAGWA


HARARE, ZIMBABWE

SIKU moja tu kabla ya Wazimbabwe kupiga kura kumchagua rais wao, Rais wa zamani Robert Mugabe, ambaye aling’olewa Novemba mwaka jana amejitokeza kusemaq hatompigia kura mrithi wake, Emmerson Mnangagwa.

Katika mkutano wa kwanza wa wazi na wanahabari tangu ang’olewe kutoka madarakani, Mugabe (94), alizungumza taratibu lakini alionekana kuwa na afya njema akiwa ameka kitini mwake nje ya makazi yake ya kifahari mjini hapa.

Wazimbabwe wanatarajia kupiga kura leo katika uchaguzi wa kwanza tangu jeshi limlazimishe Mugabe kujiuzulu baada ya miaka 37 madarakani huku kukiwa na tuhuma za wizi wa kura na wasiwasi wa utata wa matokeo.

Rais Mnangagwa, mshirika wa zamani wa Mugabe katika Chama tawala cha ZANU-PF, anakabiliana na Kiongozi wa upinzani, Nelson Chamisa wa Movement for Democratic Change (MDC) katika uchaguzi wa kihistoria katika taifa hilo la kusini mwa Afrika.

‘Siwezi kuwapigia kura wale walionidhalilisha,” Mugabe alisema, akigusia kuwa anaweza kuipigia kura MDC.

‘Siwezi kuipigia kura ZANU-PF… nini kilichobakia? Nadhani ni Chamisa tu,” alisema.

Majenerali wa Jeshi la Zimbabwe waliishtua dunia mwaka jana wakati walipochukua udhibiti wa nchi na kumweka Mnangagwa madarakani baada ya Mugabe kutuhumiwa kujaribu kumwandaa mkewe Grace (53) kuwa mrithi wake.

“Yalikuwa mapinduzi kabisa, huwezi kuingiza vifaru bila jeshi lako na vikosi kumiminwa mitaani,” Mugabe alisema na kuongeza ulikuwa upuuzi kabisa kudai alitaka Grace amrithi.

Mnangagwa (75), ambaye aliahidi mwanzo mpya kwa taifa hilo, anapewa nafasi kubwa ya kuwa rais akiwa na faida ya kuungwa mkono na jeshi, vyombo vya habari vya serikali na chama tawala kinachodhibiti rasilimali za serikali.

Lakini Chamisa (40) ambaye alifanya vyema katika mikutano ya kampeni, ana matarajio ya kupata kura nyingi kutoa kwa vijana, ambazo zinaweza kuleta mabadiliko kwa sababu ZANU-PF imetawala tangu uhuru kutoka kwa ukoloni wa Kiingereza mwaka 1980.

Wakati wa utawala wa kiimla wa Mugabe, chaguzi zilitawaliwa na machafuko na wizi wa kura na kampeni za mwaka huu ingawa zilitawaliwa na amani lakini pia tuhuma za wasiwasi wa wizi wa kura.

Chama cha MDC jana kililalamika kuwapo utata katika daftari la wapiga kura, karatasi za kupiga kura, wapiga kura kutishwa na upendeleo wa Tume ya Uchaguzi Zimbabwe (ZEC).

Hata hivyo, Mnangagwa, ambaye alituhumiwa wakati wa utawala wa Mugabe kutumia mbinu za kikatili kumdumisha madarakani, ameahidi uchaguzi huru na wa haki

Wakati uchaguzi huo ukiwa mgumu kura ya maoni ya Afrobarometer imempatia Mnangagwa asilimia 40 ya kura na Chamisa asilimia 37 huku asilimia 20 wakiwa bado kuamua.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles