25.4 C
Dar es Salaam
Monday, January 30, 2023

Contact us: [email protected]

MUGABE ATIMIZA MIAKA 93, EU IKIMWONGEZEA VIKWAZO

HARARE, ZIMBABWE


RAIS wa Zimbabwe, Robert Mugabe, amesherehekea kutimiza umri wa miaka 93 jana huku Umoja wa Ulaya (EU) ukipiga kura kumwongezea vikwazo.

Licha ya umri mkubwa na kuzidi kudhoofu kwa afya yake, Mugabe aliye madarakani tangu 1980, ameapa kuendelea kuongoza huku chama chake cha ZANU-PF kikimtangaza kuwa mgombea wake wa urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.

Kiongozi huyo mwenye umri mkubwa kuliko wote duniani kwa sasa, alitarajiwa kujumuika katika sherehe ya faragha na ndugu, jamaa, baadhi ya maofisa wakuu wa chama na Serikali na wafanyakazi wake wa karibu.

Sherehe kubwa rasmi inayotarajiwa kugharimu zaidi ya dola milioni moja, itaandaliwa siku ya Jumamosi.

Mugabe aliyezaliwa Februari 21, 1924, kwa miaka mingi ameripotiwa kutoa tembo, nyati na swala kwa ajili ya karamu.

Wakati akisherehekea kutimiza miaka 93, EU imepiga kura kuongeza vikwazo dhidi yake vikihusu kusafiri, kuzuiliwa kwa mali yake na kupiga marufuku biashara ya silaha baina yake, mkewe na Wizara ya Ulinzi ya Zimbabwe na mataifa wanachama wa EU.

Hata hivyo, EU ilipiga kura kuondoa sehemu ya marufuku ya ununuzi wa silaha dhidi ya Zimbabwe na pia imeondoa amri ya kuzuia uagizaji nje wa vilipuzi vinavyotumika kwa uchimbaji wa madini na ujenzi wa miundombinu.

Vikwazo hivyo vitatathminiwa upya mwakani.

EU ilimwekea Mugabe vikwazo mara ya kwanza mwaka 2002 baada ya kuvamiwa kwa mashamba yaliyomilikiwa na Wazungu, tuhuma za wizi wa kura pamoja na ghasia na ukandamizaji wa wapinzani na watetezi wa haki za binadamu.

Rais Mugabe anasema vikwazo hivyo vimesababisha madhila yasiyo na kifani kwa nchi yake, na kwamba ni sehemu ya mpango wa Uingereza kutaka kumwondoa madarakani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles