Mugabe amezeeka, aondoke madarakani-Rais Khama

0
1357
Robert Mugabe
Robert Mugabe

GABORONE, BOTSWANA

RAIS wa Botswana, Ian Khama, amemtaka rais mwenzake wa Zimbabwe mwenye umri wa miaka 92, Robert Mugabe, ang’atuke mara moja na kuruhusu uongozi mpya katika nchi ambayo inakabiliwa na matatizo ya kisiasa na kiuchumi tangu mwaka 2000.

Pamoja na sifa yake kama mmoja wa viongozi wenye msimamo mkali barani Afrika kauli ya Khama inatarajia kuichefua Serikali ya Zimbabwe ambako chama tawala cha ZANU-PF kiko katika mpasuko wa kuwania kumrithi.

Alipoulizwa na Shirika la Habari la Reuters iwapo Mugabe ambaye aliingia madarakani baada ya taifa hilo kupata uhuru kutoka kwa Uingereza mwaka 1980, akubali ukweli kwamba amezeeka na astaafu, Khama mwenye umri wa miaka 63 alijibu: “Bila shaka. Na alipaswa kufanya hivyo miaka mingi iliyopita.”

“Wana watu wengi wenye sifa ya uongozi ambao wanafaa kumrithi,” Khama, mzaliwa wa Uingereza, mtoto wa Rais wa kwanza wa Botswana, Seretse Khama na mkewe Mwingereza, Ruth, aliendelea.

“Ni wazi kwa umri wake na hali halisi ilivyo Zimbabwe, hawezi kutoa uongozi utakaoinasua kutoka machungu iliyonayo sasa,” Khama alisema katika kauli ambayo inakiuka msingi wa diplomasia ya Afrika, unaokataza kukosoa viongozi wenzako hadharani.

Botswana, mzalishaji mkubwa wa madini ya almasi duniani inayochangia mpaka wenye urefu wa maili 500 na Zimbabwe imeathirika na anguko la uchumi la jirani yake huyo tangu kutokea mkwamo wa kisiasa na mfumuko mkubwa wa bei mwaka 2000.

Botswana ni makazi ya Wazimbabwe 100,000 ikiwa idadi ndogo kulinganisha na Wazimbabwe milioni tatu waliopo Afrika Kusini, lakini idadi hiyo imeathiri uwezo wa Botswana kutoa huduma za umma kwa taifa hili lenye watu milioni 2.3.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here