Na Ramadhan Hassan, Mtanzania Digital
Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakari Zubeir, ametangaza kuanza ziara mkoani Dodoma kwa lengo la kukagua utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) na kushiriki mazungumzo na Waislamu wa mkoa huo. Â
Akizungumza Januari 19, 2025, jijini Dodoma katika mkutano na Masheikh wa Wilaya, Kata na viongozi wa dini ya Kiislamu, Mufti amempongeza Sheikh wa Mkoa wa Dodoma, Mustapha Rajabu, kwa uongozi bora na juhudi za kuhakikisha maendeleo ya Waislamu. Â
Mufti pia alitoa maagizo kwa Sheikh Rajabu kutuma jina la Kadhi wa Wilaya ya Mpwapwa kwa ajili ya usaili na uteuzi na kusisitiza kuwa ni muhimu Wilaya hiyo kuwa na kiongozi wa nafasi hiyo. Â
“Nakupongeza kwa kuhakikisha Wilaya zote zina makadhi, isipokuwa Mpwapwa. Tafadhali tuma jina kwa usaili ili tuhakikishe kazi inaendelea vizuri,” amesema Mufti. Â
Kwa upande wake, Sheikh Mustapha ameahidi kutekeleza maagizo yote ya Mufti kwa vitendo, akisema: “Wewe ndio kiongozi wetu, na tutahakikisha maagizo yote yanatekelezwa kwa lengo la kuimarisha maendeleo ya Waislamu,” amesema.
Aidha, Mufti amehimiza viongozi wa Bakwata kutumia baraza hilo kusimamia safari za mahujaji kwenda Makka badala ya taasisi binafsi, akieleza kuwa suala hilo litazingatiwa katika mchakato wa uchaguzi ujao wa baraza. Â
“Haiwezekani kiongozi wa Bakwata kutumia taasisi binafsi badala ya taasisi ya baraza. Tunapoelekea uchaguzi, hili litakuwa moja ya vipimo vya uadilifu wenu,” amesisitiza. Â
Ziara hiyo inatarajiwa kuimarisha mshikamano miongoni mwa Waislamu na kuchochea utekelezaji wa miradi ya maendeleo chini ya Bakwata. Â