29.2 C
Dar es Salaam
Friday, September 20, 2024

Contact us: [email protected]

Mufti Simba afariki dunia

simba 2NA SHABANI MATUTU, DAR ES SALAAM
SHEIKH Mkuu wa Tanzania, Mufti Shaaban Issa bin Simba (78), amefariki dunia jana asubuhi katika Hosptali ya TMJ, jijini Dar es Salaam.
Kifo hicho cha Mufti Simba ni pigo kubwa kwa Waislamu na taifa kwa ujumla.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum, alisema kifo cha kiongozi huyo kimetokea huku akiwa anapatiwa matibabu katika Hospitali ya TMJ.
Alisema Mufti Simba alikuwa akiugua kwa muda mrefu maradhi ya sukari na shinikizo la damu.
“Sheikh Mkuu amefikwa na umauti leo (jana) asubuhi saa moja katika Hospitali ya TMJ alikokuwa amelazwa kwa ajili ya kupewa matibabu ya maradhi ya sukari na moyo yaliyokuwa yakimsumbua,” alisema.
Sheikh Salum alisema mwili wa marehemu umetolewa Hospitali ya TMJ na kupelekwa Hospitali ya Jeshi Lugalo kwa ajili ya kuhifadhiwa.
Alibainisha kwamba Waislamu wa Jiji la Dar es Salaam walitarajiwa kukusanyika kwa ajili ya kufanya mkesha wa kumsomea dua katika eneo la Makao Makuu ya Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata), Kinondoni.

WOSIA WAKE
Wakati Bakwata wakitoa kauli hiyo, mtoto wa marehemu Suleiman Issa, alisema baba yao atazikwa leo mkoani Shinyanga.
Alisema uamuzi huo umefikiwa na kikao cha familia pamoja na kuzingatia wosia wa marehemu.
“Mwili wa marehemu utasafirishwa leo (jana) kwenda Shinyanga na kuzikwa kesho (leo) saa 10. Na hili linatokana na wosia aliouacha marehemu kwa mke wake ambaye alitaka pindi atakapofariki asicheleshwe kuzikwa,” alisema Issa.

ALIVYOANZA KUUGUA 2008
Juni 13, mwaka 2008, Mufti Simba alirejea nchini akitokea India alikokuwa akitibiwa, ambapo alifanyiwa upasuaji mkubwa wa mguu wa kulia ambao ulikatwa.
Akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya Bakwata, Mufti Simba, alisema akiwa hospitali nchini India, alifanyiwa upasuaji mkubwa baada ya mguu wake wa kulia kuoza kutokana na kushambuliwa na bakteria, ambao awali alisema hajui namna walivyoingia mguuni.
Hata hivyo, baadaye alisema ana wasiwasi huenda bakteria hao waliingia kupitia majeraha mengi aliyokuwa nayo mguuni.
“Nimerudi, ni mzima, nina afya njema, nina uwezo wa kula na madaktari wana matumaini,” alisema Mufti Simba ambaye hata hivyo alikanusha uvumi kwamba amekatwa mguu, ingawa hakuuonyesha kwa viongozi wala waandishi wa habari waliohudhuria mapokezi hayo.
“Nimepewa miezi mitatu ya mapumziko nisifanye kazi ngumu, baadaye nitarudi India,” alisema Mufti Simba.

JK AMLILIA
Rais Jakaya Kikwete, ametuma salamu za rambirambi kwa Waislamu wote nchini na Bakwata kutokana na kifo cha Mufti Simba.
Amemwelezea marehemu kama mwalimu katika jamii ambaye alikuwa na uzoefu wa hali ya juu na mwenye kupenda dini yake na kuitumia kwa manufaa ya jamii iliyomzunguka.
“Kifo kinaleta huzuni, hata hivyo kifo hakizuiliki, hatuna budi kukikubali na ni wajibu wetu kumwombea Sheikh Mkuu kwa Mola wetu ampe mapumziko ya milele,” alisema Rais Kikwete katika salamu zake za rambirambi kupitia kwa Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Salum.
“Nawaombea subra wana familia, ndugu, jamaa, Waislamu wote na wanajamii kwani Mufti alikuwa kiongozi katika jamii yetu. Kamwe mchango wake hautasahaulika katika jamii yote kwa ujumla na hakika sote tutamkumbuka,” alisema Rais Kikwete katika taarifa yake iliyotumwa na Ikulu.
Mufti Simba, alijiunga na Bakwata mwaka 1968 na amekuwa mwalimu wa chuo katika mikoa mbalimbali ikiwamo Mwanza na Bukoba na mwaka 1970 alikuwa Sheikh wa Mkoa wa Shinyanga.
Alikuwa na uzoefu mkubwa ndani ya Bakwata na aliwahi kukaimu nafasi ya Mufti kwa siku 90, baada ya kifo cha Mufti Hemed bin Jumaa bin Hemed mwaka 2002.

LOWASSA ATUMA RAMBIRAMBI
Kutokana na msiba huo mkubwa wa kiongozi huyo wa Waislamu nchini, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, ametuma salamu za rambirambi kwa Katibu Mkuu wa Bakwata, Sheikh Suleiman Lolila.
Lowassa, alisema amepokea kwa mshtuko mkubwa taarifa za kifo cha Mufti Simba.
Alisema marehemu Mufti Simba, katika uhai wake alikuwa kiungo muhimu katika kudumisha amani, upendo na mshikamano kwa taifa.
“Kifo chake si pigo kwa Waislamu tu, bali kwa Watanzania wote, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu, ambapo busara, hekima na uwezo wake mkubwa kidini vilihitajika sana.
“Nawapa pole ndugu, jamaa na Waislamu wote kwa msiba huu mkubwa. Mungu aiweke roho ya marehemu mahali pema peponi, amina,” alisema Lowassa katika taarifa iliyotumwa na msemaji wake, Elizabeth Missokia.

DK. MUKANGARA
Naye Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Mheshimiwa Dk. Fenella Mukangara, ametuma salamu za rambirambi kwa Bakwata na Waislamu wote kutokana na kifo cha Mufti Simba.
Katika salamu hizo, Dk. Mukangara amesema ni jambo la kusikitisha kumpoteza kiongozi huyo ambaye bado taifa lilikuwa likimuhitaji hasa katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu.
Waziri huyo ameongeza kuwa Mufti Simba atakumbukwa kwa upole, unyenyekevu wake na kutopenda makuu.
“Wakati wa uhai wake marehemu alikuwa tayari kumsikiliza kila mtu bila kujali dini au kabila lake,” alisema.

DK. MIGIRO
Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Asha Rose Migiro, naye ametoa pole kwa Watanzania na waumini wa dini ya Kiislamu nchini kwa kuondokewa na Shekhe Mkuu wa Tanzania, Mufti Simba.
Dk. Migiro alisema amepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha kiongozi huyo mkubwa wa dini hapa nchini.
“Natoa pole kwa wanafamilia na waumini wa dini ya Kiislamu nchini kwa kifo cha Mufti Simba. Natoa pole pia kwa Watanzania wote kwa kifo cha kiongozi muhimu katika taifa letu,” alisema.
Alisema kifo cha Mufti Simba kinadhihirisha kwamba kila nafsi itaonja mauti na kumtaka Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi.

CHADEMA WAOMBOLEZA
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema kimepokea kwa masikitiko na majonzi makubwa taarifa za msiba wa Mufti Simba.
Akitoa salamu za pole na rambirambi kwa waumini wa dini ya Kiislamu na Watanzania kwa ujumla baada ya kupata taarifa za msiba huo, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alisema Mufti Simba atakumbukwa kwa jinsi alivyokuwa akisimamia kauli zake mara kwa mara, huku akisisitiza ushirikiano ndani ya jamii ya Watanzania bila kujali tofauti zao katika itikadi za dini.
“Mara kwa mara Mufti Simba amesikika akiwaambia Watanzania – si Waislamu pekee aliokuwa akiwaongoza kiroho, hata wale wanaoamini katika madhehebu tofauti, umuhimu wa kudumisha ushirikiano miongoni mwa dini mbalimbali na makundi mengine katika jamii ikiwa ni mojawapo ya misingi ya kuimarisha umoja wa taifa letu.
“Naungana na Waislamu wote nchini katika wakati huu wa kuomboleza kifo cha kiongozi huyu wa kiroho. Kwa niaba ya uongozi wa Chadema, wanachama, wapenzi na wafuasi, natoa salamu za pole kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki, Bakwata, viongozi wa kiroho nchini na Watanzania wote ndani na nje ya nchi walioguswa na msiba huu mzito,” alisema Mbowe.
Alisema Mwenyezi Mungu awatie nguvu wote na kuwafanyia wepesi wakati huu mgumu wa majonzi ya msiba huo.

TEC WAMZUNGUMZIA
Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Raymond Saba, amesema Mufti Simba atakumbukwa na baraza hilo katika majukumu na misimamo yake katika kutekeleza mambo mbalimbali ambayo yanalenga imani za dini zote.
Alisema TEC wamepokea kifo hicho kwa mshtuko na hawana budi kumuenzi katika mambo yake mbalimbali ikiwamo mchango wake katika taifa na jamii kwa ujumla na mahusiano ya dini mbalimbali.
“Mungu ampe usingizi wa amani mzee wetu na dua njema tunamwombea, daima tutamkumbuka kutokana na kazi yake ya kuwaunganisha waumini wa dini zote kwa pamoja, hili ni pigo kwetu na Baraza la Waislamu Tanzania kwa ujumla,” alisema Saba.
Aliongeza kuwa mambo mazuri aliyoyafanya Mufti Simba yanafaa kuenziwa na jamii nzima kwani alikuwa ni kiongozi asiyependa kuyumbishwa na mwenye misimamo thabiti, yenye nia ya kujenga dini imara na kuwakutanisha Waislamu na Wakristo kwa pamoja.
Pia aliwaomba waumini wa dini mbalimbali kushirikiana kwa pamoja kumwombea Mufti Simba katika safari yake mpya aliyoianza.

HISTORIA YAKE BAKWATA
Alichaguliwa kuwa mufti mwaka 2002, baada ya kifo cha mtangulizi wake, Sheikh Hemed bin Jumaa bin Hemed.
Katika kinyang’anyiro cha uchaguzi huo uliofanyika mjini Dodoma katika Chuo cha Biashara (CBE), kulikuwa na ushindani mkubwa kati yake na marehemu Sheikh Sulemani Gorogosi pamoja na Profesa Juma Mikidadi.
Sheikh Gorogosi alifariki dunia Juni 27, mwaka 2009.
Moja ya kauli kubwa ambayo itakumbukwa ya Mufti Simba baada ya kumalizika kwa mkutano huo wa uchaguzi, ni ile aliyowaeleza wajumbe waliohudhuria kuwa ‘vichwa visivyosikia atavipiga marungu’ iliyokuwa ikiwalenga wale waliokuwa wakiivuruga Bakwata.
Mwaka 2006, Mufti Simba aliahidi kuifanyia mabadiliko makubwa Bakwata ili iweze kuwanufaisha Waislamu wote nchini.
Akizungumza baada ya Swala ya Ijumaa katika Msikiti wa Mtoro, jijini Dar es Salaam, alisema kumekuwapo na malalamiko mengi yanayowahusu baadhi ya viongozi wa baraza hilo na aliahidi kuchukua hatua za kulisafisha.
Mufti Simba pia aliahidi kuufanyia marekebisho muundo wa baraza hilo, kurekebisha Idara ya Elimu, kuanzisha Mfuko wa Mufti kwa ajili ya kusomesha yatima na wajane pamoja na ujenzi wa ofisi za kisasa makao makuu ya baraza hilo – ambao tayari umetekelezwa.
Bakwata iliyomilikishwa na Serikali mali za iliyokuwa Taasisi ya Waislamu ya Afrika Mashariki (East Africa Muslim) mwaka 1968, ni moja ya taasisi za kidini nchini iliyopata bahati ya kumiliki mali na vitegauchumi vikubwa.

Habari hii imeandaliwa na Shabani Matutu, Aziza Masoud na Christina Gauluhanga, Dar es Salaam

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles