BENJAMIN MASESE-MWANZA
MUFTI wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir, amewataka Waislamu kushindana kuujenga Uislamu kuwa kielelezo na mfano ndani ya jamii na si kuchafuana na mfarakano ambao unawagawa waumini.
Kauli hiyo aliitoa juzi wakati akizindua msikiti wa kisasa wa Masjid Nnabawiyya-Kanindo jijini Mwanza.
Mufti alisema ameshangazwa namna uwekezaji mkubwa uliofanywa na mali za mume na mke kwa kujenga msikiti huo na kuukabidhi Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata).
Alisema msikiti huo umekuwa msaada, hususan kwa waumini wa Kiislamu ambao walikuwa wakitembea kilomita 10 kufuata huduma ya kuabudu, hivyo kitendo hicho ni kielelezo tosha cha umoja wao ndani ya jamii, kumtii na kumshika mkono Mwenyezi Mungu.
“Nilipoambiwa na Sheikh wa Mkoa, Hassan Kabeke kwamba katika ziara yangu Mkoa wa Mwanza nitazindua msikiti nilisita kidogo, kwa sababu sikujua nitakuta kitu kama hiki, fikra zangu zilinielekeza ni msikiti wa kawaida, lakini nilipofika hapa nilishangaa, mpaka sasa siamini kabisa umejengwa na mume na mke kwa mali zao.
“Huu ndio Uislamu imara na wenye kumtii Mungu, hakika waumini hawa wamefanya jambo kubwa ndani ya jamii, Mungu awalipe malipo makubwa kwa kazi hii ya kutumia nusu ya mali zao kumshika mkono Mwenyezi wetu, wote tukiwa hivi nadhani tutakuwa mfano wa kuiga kwa wengine, wito wangu kwa Waislamu tuache kuleta mfarakano, badala yake tuungane tujenge Uislamu wa kweli,” alisema.
Kwa upande wake, Sheikh Sefu Omari aliyejenga msikiti huo, alisema kuwa aliamua kujenga msikiti, shule na maduka ya biashara kwa fedha zake mwenyewe kwa kusaidiana na mke wake baada ya kuona jamii ya Mtaa wa Kanindo inakosa huduma ya kuabudu karibu na wanapoishi.
Alisema baada ya ujenzi huo waliamua kukabidhi msikiti Bakwata na kubakiwa na shule na maduka ambayo yanaendelea kuwaingizia kipato.
Aliiomba jamii, hususan Waislamu kuachana na watu wanaochafua msikiti huo kwa kuuhusisha na imani za kishirikina.
“Huu msikiti ni wa Watanzania wote, hasa Waislamu, nimeujenga hapa kwa ajili ya jamii inayoishi hapa na wengine wanaopenda kuja kuswali hapa, ndiyo maana nimeukabidhi Bakwata, nashangaa kuna watu wanasema hapa kuna majini, sasa nahoji leo kiongozi wetu mkuu nchini ameswali hapa je, amepatwa na majini?
“Naomba watu waache fitina, hasira, chuki na kuleta mgawanyiko ndani ya Uislamu, tupo duniani kwa maisha mafupi sana, hivyo tutumie muda wa uhai wetu kupendana.
“Wito wangu nawaomba waumini wa Kiislamu waje tuswali hapa hapa na hakuna chochote kitakachowapata,” alisema.
Naye Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Hassan Kabeke alisema tayari wamejiwekea mipango yao ya kuendeleza na kuisimamia misikiti inayokabidhiwa Bakwata ili iweze kuendelea kutoa huduma kwa waumini wake.
“Baada ya kukabidhiwa msikiti huu, nimeleta wataalamu hapa kuendeleza baadhi ya mambo kama kutoa elimu ya madrasa kwa wanafunzi, kikubwa kwa kuwa katibu mkuu upo hapa, nitaleta maombi yangu, naomba yakifika mezani yapewe kipaumbele,” alisema.
Akihutubia waumini wa Kiislamu na wananchi baada ya uzinduzi huo, Mjumbe wa Baraza la Maulamaa Taifa, Alhaji Hamid Jongo alisema kitendo cha kujenga msikiti wa kisasa na kuukabidhi Bakwata ni Uislamu halisi na tendo la kumtii mwenyezi Mungu.
“Ni jambo lisilo la kificho, hapa Omari amemshika mkono Mungu na atapokelewa na kumuona Mwenyezi, naomba Waislamu washindane katika kuujenga Uislamu na vitu vinavyoonekana kwa macho ili watoto na jamii iweze kufaidi mbeleni,” alisema.