MUFTI AKABIDHIWA EKA 50

0
504

NA MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM


WAUMINI wa dini ya Kiislamu, wametakiwa kujitolea kwa namna mbalimbali katika kuchangia maendeleo yao na Watanzania kwa ujumla.

Mufti wa Tanzania, Sheikh Mkuu Abubakar Zuberi bin Ally, alisema hayo Dar es Salaam jana, wakati akipokea hati ya umiliki wa kiwanja cha eka 50 kilichopo mkoani Ruvuma kutoka kwa mmoja wa viongozi wa Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata), mkoani humo, Ali Mahaba.

Alisema eneo hilo lenye hati ya umiliki wa miaka 99, bado halijapangiwa matumizi, lakini huenda likatumika kujenga shule, hospitali au jengo la kitega uchumi.

“Tuangalie Uislamu una kiu gani kwa wakati huu, tuna kiu ya elimu, afya, uchumi na maendeleo yote kwa ujumla.

“Uislamu unajengwa na masheikh, matajiri, masikini na wote wenye mapenzi mema, nawahakikishia Bakwata hatutawaangusha, tutayafanyia kazi ipasavyo yote mnayojitolea pamoja na michango yenu,” alisema Mufti.

Akizungumza baada ya kukabidhi hati hiyo, Mahaba alisema mabadiliko ya kiuongozi ndani ya Bakwata ndiyo yaliyowashawishi viongozi wa Ruvuma kuchangia ardhi hiyo kwa maendeleo.

“Tuna imani na wewe, una mvuto katika elimu na kuleta mabadiliko ndani ya sekta hii, tumeona iko haja tukupe zawadi isije kuonekana tunasema tu, lakini hakuna mtu nyuma yako.

“Endelea na juhudi zako za kuupeleka mbele Uislamu, hasa katika ile tume ya kufuatilia mali za Waislamu,” alisema Mahaba.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here