29.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

MUDA WA KUPOKEA KODI YA MAJENGO WAONGEZWA TENA

Mkurugenzi wa Idara ya Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo

Na Aziza Masoud – Dar es Salaam

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imeongeza muda wa kupokea kodi za majengo za mwaka 2016/17 hadi Julai 30 mwaka huu na zaidi imetangaza kutoa  adhabu kwa yeyote atakayekaidi agizo hilo.

Katika kuhakikisha ulipaji huo haukwami, TRA imesema Mkoa wa Dar es Salaam umetengewa vituo maalumu 12 kutekeleza  hilo.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Idara ya Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo, alisema ulipaji huo ambao ulipaswa kukamilika jana, umeongezewa muda kutokana na mwitikio mkubwa wa wananchi.

“TRA inapenda kuwatangazia wamiliki wote wa majengo kuwa itaendelea kutoa huduma ya ukusanyaji wa kodi ya majengo katika ofisi za TRA nchi nzima, kwa Mkoa wa Dar es Salaam tutaendelea kukusanya kodi hizo katika vituo maalumu hadi kufikia Julai 30 bila adhabu,” alisema Kayombo.

Alisema vituo vitakavyotumiwa kukusanya kodi kwa Dar es Salaam ni pamoja na Viwanja vya Maonyesho ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) na ofisi za TRA zilizopo maeneo mbalimbali ikiwamo Mbagala.

Alisema huduma hiyo pia itapatikana katika ofisi za TRA Temeke Maduka Mawili, Kigamboni, jengo Millenium Tower, Tegeta, Kimara, Manzese, Ilala, Gerezani, Vingunguti na Samora.

Kayombo alisema TRA pia imeanza kupokea kodi ya malipo hayo kwa mwaka 2017/18.

Alisisitiza wamiliki wote wa majengo wana wajibu wa kisheria wa kulipa kodi hiyo,  hivyo wanapaswa kufika katika ofisi hizo  kuchukua hati za madai na kufanya malipo.

Akizungumzia kuhusu malalamiko ya watu kutozwa fedha za malipo ya nyumba mbili katika kiwanja kimoja, alisema mamlaka inahesabu majengo na si eneo.

“Tunahesabu majengo yaliyo ndani ya kiwanja na si eneo, tukifanya uthamini tunahesabu hadi ukuta ni sehemu ya jengo,” alisema Kayombo.

Alisema kwa nyumba za kawaida ambazo hazijawahi kuthaminiwa, wanapoanza kujaza fomu watalipa Sh 10,000 wakati nyumba ya ghorofa kila ghorofa inalipiwa Sh 50,000.

Akizungumzia kuhusu msamaha uliotolewa kwa wazee wenye nyumba za kuishi, alisema ili kupata msamaha wanapaswa kufuata taratibu tatu.

“Ili mzee apate msamaha wa kodi anapaswa kuandika barua ya kujieleza kuomba msamaha wa kodi, awe na barua ya utambulisho kutoka Serikali za mitaa, uthibitisho wa barua ya kustaafu,” alisema Kayombo.

Alisema kwa sasa mamlaka bado haijaanza kuhudumia wazee kutokana na uwepo wa foleni za walipaji hao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles