27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

MTV MAMA 2016 Black Coffee kwenye ubora wake, Diamond upo?

 diamond123

Na CHRISTOPHER MSEKENA,

WIKI hii uongozi wa kituo cha runinga cha MTV Base kinachoandaa Tuzo za MTV Africa Music Awards (MTV MAMA 2016) kilitangaza majina ya mastaa wa muziki Afrika ambao wameingia kwenye kinyang’anyiro cha tuzo hizo mwaka huu.

Tuzo hizo kubwa zenye heshima ya aina yake Afrika huwa zinavuka mipaka ya bara hili na kuwasogeza karibu wasanii wakubwa kutoka  mabara mengine kama vile Marekani na Ulaya na mwaka huu mastaa kama Drake, Beyonce, Adele, Future na Rihana wamekutanishwa kwenye kipengele cha Msanii Bora wa Kimataifa.

Sherehe za utolewaji wa tuzo hizi zinatarajiwa kufanyika huko Johannesburg, Afrika Kusini, Oktoba 22, mwaka huu na burudani juu ya jukwaani itasimamiwa na Patoranking, Kwesta, Diamond Platnumz, Emtee, Ali Kiba, Cassper Nyovest na Ycee.

Kama kawaida Bongo Fleva haipo nyuma ambapo mwaka huu wasanii wake watatu wameingia kwenye kinyang’anyiro cha tuzo hizo. Hao si wengine bali ni Ali Kiba, Navy Kenzo na Diamond Platnumz.

Kiba, ambaye pia atatumbuiza yupo kwenye kipengele cha Wimbo Bora wa Kushirikiana (Best Collaboration) kupitia wimbo alioshirikiana na Kundi la Sauti Sol unaoitwa Unconditionally Bae, tuzo inayowaniwa na wasanii wengine kama vile AKA, Nasty C, Patoranking na DJ Maphorisa.

Kwa mara ya kwanza kundi linaloundwa na wapenzi, Aika na Nahreel limeendelea kudhihirisha ubora wake kwani safari hii limeweza kupenya na kuingia kwenye tuzo hizi zenye ushindani mkubwa.

Kundi hilo linalofanya poa na ngoma yake ‘Kamatia Chini’ lipo kwenye Kipengele cha Kundi Bora (Best Group). Tuzo hii pia ina ushindani wa aina yake kwa sababu inayakutanisha makundi mengine yaliyofanya vizuri mwaka huu.

Makundi kama Micasa, Toofan, R2bees na Sauti Sol yanaweza kuwapa changamoto Navy Kenzo, ila kura yako wewe shabiki wa Bongo Fleva inaweza ikafanya maajabu, Navy Kenzo wakaondoka na tuzo hiyo mwaka huu.

Mbali na Navy Kenzo na Ali Kiba kuwania tuzo hizi, tena ikiwa ni mara yake ya pili kuingia kwenye tuzo hizo, big boss wa WCB, Diamond Platnumz mbali na kutumbuiza ana changamoto ya kuviruka vizingiti vya mastaa wengine waliopo kwenye kipengele cha Msanii Bora wa Kiume (Best Male).

Achana na kina AKA, Patoranking na Wizkid ambao ni levo yake na anawamudu, kuna kigingi kingine cha kahawa nyeusi au Dj Black Coffee ambacho ni kikongwe na cha kuogopwa kwenye tuzo hii kulingana na sifa zake kwenye muziki wa Afrika.

Hii inakuwa mara ya pili kwa Diamond kukutana na Black Coffee. Nadhani unakumbuka jina la mchezeshaji huyu wa muziki lilivyokua ghafla kwenye masikio ya mashabiki pale ambapo Diamond alitoka jasho bila mafanikio kwenye tuzo za Black Entertaiment (BET) zilizofanyika Los Angeles, Marekani mwezi Juni, mwaka huu.

Dj Black Coffee ambaye ni mlemavu wa mkono wa kushoto aligeuka kuwa mada inayozungumzwa zaidi na Watanzania hasa kwa wale  ambao waliweka matumaini ya ushindi Diamond, Wizkid, Yemi Alade, AKA, MzVee, Cassper Nyovest na Serge.

Ukanda wa Afrika Mashariki ulikuwa haumfahamu sana Dj Black Coffee ila ushindi wake uliochangiwa na kushindwa kwa Diamond aliyekuwa anaiwakilisha Afrika Mashariki basi alifanikiwa kujizolea mashabiki wa kutosha.

Lakini kabla kidonda cha kuikosa tuzo ya BET hakijapona sawasawa, Diamond  anakutana tena na Dj huyu.

Je, anaweza kuchomoka na tuzo au atabanwa mbavu? Kama kigezo kikiwa ni wingi wa kura na wewe Mtanzania ukipiga kura kwa wingi basi  Diamond na washiriki wengine kutoka Tanzania wataweza kuibuka na tuzo hizo.

Piga kura sana kwa ajili yao; Diamond, Ali Kiba na Navy Kenzo. Kila la kheri mashujaa wetu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles