Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MWANDISHI wa tamthilia ya ‘Ngoswe kitovu cha Uzembe’, Edwin Semzaba, amefariki dunia juzi jijini Dar es Salaam.
Taarifa ya kifo hicho ilianza kuenea juzi usiku katika mitandao ya kijamii ambapo Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Rwekaza Mukandala, alithibitisha kifo hicho.
“Ni kweli amefariki ila anayeweza kuzungumzia hilo vizuri ni Ofisa Uhusiano wetu Walter Luanda ambaye yupo katika eneo la msiba hivi sasa,” alisema Profesa Mukandala.
Alipotafutwa Luanda, alisema yupo kwenye eneo ambalo si zuri ila apigiwe simu baada ya dakika 10, lakini baada ya muda huo simu yake ilipopigwa haikupokewa.
Wakati wa uhai wake, Semzaba aliandika tamthilia ya Ngoswe akiwa kidato cha tatu.
Kutokana na kipawa alichopewa na Mwenyezi Mungu, aliweza kuihifadhi hadi baadaye ilipokuja kuchezwa na Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD) kabla ya kubadilishwa na kuitwa TBC Taifa.
Semzaba ni miongoni mwa waandishi wachache waliokuwa hazina ya Kiswahili nchini.