27.1 C
Dar es Salaam
Thursday, December 7, 2023

Contact us: [email protected]

Mtuhumiwa ugaidi azua jambo kortini

Arusha Town
Arusha Town

NA ELIYA MBONEA, ARUSHA

WATUHUMIWA wa kesi ya ugaidi na kufanya uwakala wa kusajili vijana kujiunga na kundi la Al-Shabaab la nchini Somalia, wametaka upande wa mashtaka uwaeleze alipo mtuhumiwa mwenzao, Abdallah Thabit.

Malalamiko hayo yalitolewa jana mbele ya Hakimu Mkazi, Rose Ngoka, wakati kesi hiyo ilipokuwa ikitajwa.

Wakati watuhumiwa hao wakiwa mbele ya hakimu huyo, mtuhumiwa Ally Hamis alinyoosha mkono na kumuomba Hakimu Ngoka amsaidie kuuliza upande wa mashtaka ni kwanini mtuhumiwa mwenzao huyo hakufikishwa mahakamani hapo.

“Mheshimiwa hakimu, Julai 24 mwaka huu, upande wa mashtaka ulidai ungemleta mtuhumiwa Thabit, lakini mpaka leo hatujui ni kwanini hajaletwa mahakamani,” alihoji Hamis.

Akijibu hilo, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Gaudencia Joseph, aliiambia mahakama kwamba hakuwa na taarifa za mshtakiwa huyo kutofikishwa mahakamani.

Kutokana na hali hiyo, aliomba apewe muda ili afuatilie suala hilo.

Hamis alionekana kutoridhishwa na majibu hayo, na akaieleza mahakama kwamba yalitolewa na mwendesha mashtaka Julai 24, mwaka huu wakati walipofikishwa mahakamani hapo.

Mvutano huo ulimfanya Hakimu Ngoka aingilie kati na kudai kuwa majibu sahihi yangetakiwa kutolewa na mwendesha mashtaka anayelifahamu suala hilo vizuri na si mwendesha mashtaka Joseph.

“Tatizo ni kwamba hakimu na mwendesha mashtaka katika shauri hili wote hawapo. Kwahiyo, tunaliahirisha hadi Septemba 3, mwaka huu,” alisema Hakimu Ngoka.

Katika hatua nyingine, mtuhumiwa Abdallah Athumani alihoji ni kwanini upelelezi wa kesi umechelewa kukamilika ingawa waliwahi kuelezwa ungechukua siku 60.

“Mheshimiwa hakimu, tunaiomba mahakama yako itusaidie juu ya hili, hivi ni kwanini upelelezi haujakamilika wakati tuliwahi kuambiwa ungechukua siku 60 na baadaye tukaambiwa upelelezi hauna muda maalumu?” alihoji.

Akijibu hilo, mwendesha mashtaka Joseph aliiambia mahakama hiyo kwamba mwendesha mashtaka halisi katika shauri hilo hakuwa mahakamani, na kwamba hakuwa na majibu ya kutosha kwa kuwa yeye alihusika katika kesi hiyo kwa ajili ya kuiahirisha.

“Mwendesha mashtaka anayehusika na shauri hili siyo mimi, nawaomba wasubiri hadi Septemba 3, mwaka huu kesi hii itakapotajwa tena kwani siku hiyo mhusika halisi atakuwapo,” alisema Joseph.

Katika kesi hiyo, washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka ya kuua, kujaribu kuua, kusajili na kusafirisha vijana kwa ajili ya kujiunga na kundi la Al-Shabaab.

Pia watuhumiwa hao wanahusishwa na mlipuko wa bomu lililotokea katika baa ya Arusha Night Park jijini Arusha na kusababisha kifo cha mtu mmoja na kujeruhi wengine 16.

Washtakiwa hao ni Abdallah Athumani, Abdallah Thabit, Ally Hamisi, Abdallah Wambura, Rajabu Hemedi, Hasani Saidi, Ally Hamisi, Yasini Sanga, Shaabani Wawa, Swalehe Hamisi, Abdallah Yasini, Abdallah Maginga na Sudi Nasibu Lusuma.

Wengine ni Shabani Musa, Athuman Hussein, Mohamed Nuru, Jafari Lema, Abdul Mohamed na Said Michael Temba.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles