25.9 C
Dar es Salaam
Thursday, December 8, 2022

Contact us: [email protected]

Mtuhumiwa mauaji ya albino akutwa na mkono

Na Clara Matimo, Mwanza

Jeshi la polisi Mkoa wa Mwanza linawashikilia watu watano kwa tuhuma za kuhusika na kifo cha kikatili cha Joseph Mathias (28) mwenye ualbino aliyekuwa mkazi Kata na Tarafa ya Ngulla Wilaya ya Kwimba mkoani humo kilichotokea usiku wa Novemba 2, 2022 kwa kukatwa mkono wa kulia na kusababisha kifo chake.

Kati ya watu hao mtu mmoja ambaye jina lake limehifadhiwa alikamatwa akiwa na mkono wa binadamu ambao  unadhaniwa ni wa mtu mwenye ualbino akiwa ameuhifadhi ndani ya begi jeusi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa(aliyesimama) akitoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima(wa pili kushoto) mbele ya waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu kukamatwa kwa watuhumiwa wa mauaji ya mtu mwenye ualbino.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa amebainisha hayo  Novemba 8, wakati akitoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima mbele ya waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa agizo alilolitoa kwa jeshi hilo Novemba 3, mwaka huu la kulitaka liwasake na kuwakamata wahusika wote wa mauaji hayo ndani ya wiki moja alipofika katika msiba wa Joseph na kuwapa pole familia ya marehemu huyo.

Kamanda Mutafungwa alieleza kwamba  watuhumiwa hao waliwakamata Novemba 6, 2022 baada ya jeshi hilo kufanya msako mkali kwenye maeneo mbalimbali katika wilaya zote zilizopo mkoani Mwanza ikiwemo  kuwashirikisha wananchi watoe taarifa endapo watabaini taarifa yoyote itakayosaidia watuhumiwa kukamatwa.

“Novemba 6, 2022 saa sita mchana mtu mmoja mwanaume mkazi wa Kijiji cha Gambajiga, Kitongoji cha Itungwa, Kata ya Kanyelele, Tarafa ya Usagara Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza alionekana akiwa  na wasiwasi akiwa amebeba begi lenye rangi nyeusi ambalo linatoa harufu kali isiyo ya kawaida  akitafuta mganga wa kienyeji ili kwenda kujisafisha kutokana na tukio baya alilokuwa amelifanya ambalo wanachi aliowauliza hawakujua kwa wakati huo ni tukio gani.

“Wananchi walilitilia shaka begi hilo, mara moja walitoa taarifa polisi waliokuwa Kata ya Kanyelele. Askari walipofika na kupekua begi hilo walikuta mkono wa binadamu wa upande wa kuume ukiwa umeoza na unatoa harufu kali. Pamoja na ushahidi ambao tayari tumeupata kuonesha kwamba mkono huo ni kiungo kilichokatwa kutoka kwa marehemu Mathias, jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa kitaalamu zaidi unaoshirikisha Ofisi ya Mkemia Mkuu.

Alisema jeshi la polisi linaendelea kumhoji mtuhumiwa huyo kuhusiana na tukio hilo na anaendelea kushirikiana na Jeshi la polisi katika kuwakamata wahusika wote walioshiriki  kufanya tukio la  kikatili ambalo limeacha huzuni kwa familia ya marehemu na jamii kwa ujumla.

“Mtakumbuka Marehemu Joseph Mathias aliuawa usiku wa Novemba 2, 2022 saa tano usiku akiwa nyumbani kwake  katika Kijiji cha Ngulla ambapo usiku akiwa amelala nyumbani kwake pamoja na mkewe alisikia sauti ya mtu aliyemfahamu ikimtaka atoke nje ya nyumba ili waende kunywa pombe za kienyeji, marehemu alifungua mlango na kutoka nje, ghafla lilitokea kundi la watu waliokuwa na panga na kumshambulia kwa kukata mkono wake wa kuume na kutoweka nao baada ya tukio hilo la kikatili mhanga alivuja damu nyingi na kupoteza maisha kabla ya kufikishwa hospitali, ”alisema Kamanda Mutafungwa.  

“Natoa wito kwa wananchi kuendelea kuliamini jeshi la polisi na kusaidia kufanikisha kuwakamata wahalifu na pia natoa onyo kali kwa jamii kuacha mara moja kufanya vitendo vya kihalifu kwani watakaokaidi agizo hilo watachukuliwa hatua kali za kisheria maana lazima tutawakamata tu, pia waliohusika katika maujaji ya Mathias wote tutawakamata na kuwafikisha mahakamani” alisisitiza Kamanda Mutafungwa.

Baada ya maelezo hayo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Adam Malima alilipongeza jeshi hilo pamoja na wananchi kwa ushirikiano uliowezesha watuhumiwa hao kukamatwa huku akivitaka vyombo vinavyohusika na uchunguzi kuendelea kufuatilia mwenendo mzima wa uovu huo ili asibaki mtu  hata mmoja aliyehusika na tukio hilo bila kukamatwa.

“Nawashukuru jeshi la polisi kwa kuwakamata watuhumiwa mapema nilitoa siku saba lakini mmetekeleza ndani ya siku nne, maelekezo yangu ya pili hatujakamilisha uchunguzi kwa sababu mkono umepatikana hapana, nataka kumjua aliyeagiza huo mkono, aliyepelekewa huo mkono, nataka kumjua anayehusika kwamba tukipata mkono wa albino nitapata madini, nitapata ushindi kwenye uchaguzi, uteuzi hauwezi kuniacha naamini watuhumiwa walipoenda kumkata mkono marehemu lazima kuna myororo wa watu waliohusika kufanikisha tukio hilo nawataka wote wakamatwe,” Malima aliliagiza jeshi la polisi na kuongeza:

“Lazima kuna sababu za hovyo hovyo hapo ambazo zimesababisha Joseph auwawe, sasa mimi nimesema kila mtu aliyehusika akamatwe hata bodaboda aliyemtoa ngulla hadi Misungwi huyo mtuhumiwa aliyekutwa na mkono naye anahusika huo ni myororo haiwezi kuwa huyo aliyekamatwa na mkono wake tuseme imetosha nataka nikomeshe tabia hii ndani ya mkoa huu,”alisisitiza na kusema.

 “Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Amiri Jeshi Mkuu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameniteuwa mimi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza ahadi yangu kwa wananchi wa Mwanza ni kwamba sitaruhusu mwananchi yoyote aishi kwa mashaka kwa sababu ya rangi ya ngozi yake au kwa sababu ya ulemavu wake wowote.

“Kila mtu anahaki ya kuishi  Mwanza kwa raha zake as long as anaishi katika misingi ya sheria no problem. Novemba 3, 2022  nilipokuwa msibani kwa Joseph kulikuwa na mtoto mwenye ualbin ambaye anamiaka nane alikuwa amejawa na hofu sana anasema anaogopa kwenda shule tunaachaje watanzania wenzetu waishi kwa hofu ndani ya nchi yao  mimi sitaruhusu hilo,”alisema Malima.

Mauaji ya watu wenye ualbino yaliibuka hapa nchini mwaka 2006 ambapo yalihusisha baadhi ya matukio dhidi yao ikiwemo kukatwa viungo vya mwili na utekwaji nyara ambapo ripoti nyingi zilionesha wanauwawa kwa sababu ya  imani za kishirikina  huku watu waliokuwa wakitekeleza ukatili huo wakiamini kwamba viungo hivyo vinaweza kuwapa utajiri.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,710FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles