MTOTO WA TRUMP AKIRI KUKUTANA NA URUSI

0
440

WASHINGTON, MAREKANI


MTOTO mkubwa wa kiume wa Rais wa Marekani Donald Trump, amekiri kuonana na mwanasheria mmoja mwenye ukaribu na Ikulu ya Urusi, Kremlin.

Donald Trump Junior alikiri kuonana na mwanasheria huyo, Natalia Veselnitskaya muda mfupi baada ya baba yake kuidhinishwa kuwa mgombea urais kwa tiketi ya chama cha Republican.

Kwa kufanya hivyo, alikuwa na matumaini ya kupata taarifa zinazoweza kumsaidia baba yake katika kampeni za uchaguzi.

Likiwanukuu washauri wa Ikulu ya Marekani, gazeti la New York Times liliripoti kwamba mtoto huyo alikubali kukutana na Veselnitskaya baada ya kuahidiwa taarifa dhidi ya aliyekuwa mgombea wa Chama cha Democratic, Hillary Clinton.

Mkutano huo uliofanyika Juni mwaka jana kwenye jengo la Trump Tower, ulihudhuriwa pia na shemeji yake Jared Kushner na Paul Manafort aliyekuwa wakati huo mwenyekiti wa kampeni ya Rais Trump.

Msemaji wa kundi la wanasheria wa Trump, Mark Corallo amesema ‘Rais hakuwa na taarifa kuhusu kile kilichokuwa kikiendelea na wala hakuhudhuria mkutano huo.’

Tuhuma hizo zinajiri wakati Trump akiendelea kuchunguzwa kuwa alishinda uchaguzi wa urais wa Marekani dhidi ya Clinton kwa msaada wa Urusi, kitu ambacho anaendelea kukikana.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here