ALIYEKUWA mwimbaji wa bendi ya Vijana Jazz, Komweta Maneti, ameendelea kuandaa nyimbo zake kama msanii binafsi ili aendeleze kipaji chake tofauti na kuimba katika bendi.
Komweta amesharekodi nyimbo kadhaa chini ya prodyuza C9 aliyekuwa studio ya Kiri record na sasa anaendelea kuzikamilisha nyimbo hizo zaidi ya tano kwa ajili ya kuanza kuzitoa kwa mashabiki wake kabla ya kuanza maonyesho yake.
“Niliachana na kazi za bendi kwa ajili ya kujiimarisha mwenyewe na sasa naendelea kuzirekebisha nyimbo tano nilizorekodi ili nianze kuziachia kwa awamu kwa mashabiki wangu kama nilivyoahidi,” alisema.
Baadhi ya nyimbo hizo ni ‘Dolisamwela, Ilikuwa zamani, Walimwengu, Utanizingua, Nitajuaje na Nilikupenda’.
“Lengo langu ni kuziba pengo la baba yangu marehemu Maneti lakini kama sitoziba isikike sauti yake kama ilivyokuwa zamani maana alikuwa mtu mkubwa katika sanaa ya uimbaji nami nataka nifikie mafaniko yake kimuziki,” alieleza Komweta.