30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

MTOTO WA GADDAFI ANAWEZA KUIONGOZA LIBYA?

SEIF al-Islam Gaddafi

 

 

TRIPOLI, LIBYA

SEIF al-Islam Gaddafi (mwenye miaka 44) ameachiliwa huru kutoka jela nchini Libya baada ya miaka sita. Kwa mujibu wa taarifa ya Brigedia mmoja kutoka Kikosi cha waasi kinachoongozwa na Abu Bakr al-Sadiq na chenye makao yake mjini Zintan, magharibi mwa Libya, mtoto wa Gaddafi aliachiliwa huru, licha ya kuwa mtu anayetafutwa sana na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).

Wengi wanajiuliza nini kitakachofuata kwa mtoto huyu wa Kanali Muammar Gaddafi, ambaye wakati mmoja alionekana kukaribia kurithi wadhifa wa baba yake wa kuiongoza Libya.

Ni kweli Seif al-Islam Gaddafi yuko huru?

Kwa mujibu wa kikosi cha wanamgambo kilichokuwa kimemshikilia tangu mwaka 2011, pamoja na mmoja wa mawakili wake, ni kweli yuko huru. Hata hivyo, pande zote mbili zimewahi kusema hivyo Julai, mwaka jana. Mwishowe, iligundulika haikuwa taarifa ya kweli.

Seif anaweza kuwa hakutazamwa kama “mtu huru”, katika nadharia, katika mwaka uliopita na kikosi kilichomzuia. Lakini hakukuwa na ushahidi wakati huo na sasa, kwamba amewahi kutoka nje ya mji wa Zintan.

Kwanini ameachiliwa wakati huu?

Ni vigumu kuielewa Libya na siasa yake ya uanamgambo. Hakuna mtu anayeweza kusema hakika ni kwa nini kuachiliwa kwake kumetangazwa wakati huu, lakini baadhi wanaamini inaweza kuhusika na mgogoro unaoendelea kati ya makundi pinzani ya wanamgambo na makundi ya kisiasa.

Seif yuko wapi kwa sasa?

Jibu ni rahisi, haijulikani alipo. Hadi sasa wakili wake hajasema bayana mahali aliko mteja wake kwa sababu za kiusalama. Wapo wanaoamini kuwa kama ameondoka mji wa Zintan, inaaminiwa yupo mashariki mwa Libya.

Wengine wanaamini alikwenda kusini, na baadhi wanafikiri kuna uwezekano mkubwa wa Seif kuelekea katika mji wa Bani Walid zaidi ya mahali pengine popote. Hii ilikuwa ni moja ya maeneo ya mwisho kuanguka utawala wa baba yake wakati wa vita vya 2011. Inaelezwa wakazi wa mji huo ni wafuasi wa serikali ya zamani. Baadhi wamesema labda yupo nchini Misri.

Je, mpango wake ni upi?

Hili litakuwa swali zito mno, lakini jawabu lake kwa sasa litakuwa la kubuni. Mpango wa Seif utakuwa bayana ikiwa atatoa taarifa nini kitakachofuata baada ya kuachiliwa. Wakili wake amedai kuwa huenda Seif akawa mtu wa kutegemewa kuleta maridhiano ya kitaifa.

Je, anaweza kuingia tena katika siasa?

Nchini Libya kila kitu kinawezekana. Tangu 2011, wanachama na taasisi za serikali ya kale yamerejea mamlakani, angalau katika uwezo tofauti. Hata hivyo, kama Seif Gaddafi ataingia huenda akakabiliana na vikwazo vingi.

Je, anaweza kusafiri ndani ya Libya?

Kinadharia, ndiyo, lakini si kwa uhuru au kwa urahisi. Baadhi ya vikosi vilivyo na nguvu zaidi nchini vitakasirishwa na ripoti za kuachiliwa kwake na kuna uwezekano wa kujaribu kumkamata tena.

Nini kimetokea katika hukumu yake ya kifo?

Mahakama ya Tripoli iliyomhukumu haijaifutilia mbali na haionekani kama kuna mpango wowote wa kufanya hivyo. Mwendeshaji mkuu wa mashtaka, aliyepo Tripoli, pia haamini sheria ya msamaha iliyopitishwa na bunge mjini Zintan inafaa kutumika kwa Gaddafi.

Wanamgambo waliomwachilia walitaja sheria hii wakitangaza kuachiliwa kwake na walidai kuwa walikuwa wanafuata taratibu za kisheria.

Walibya wanafikiria nini?

Kwa baadhi, Seif Al Islam Gaddafi daima atakuwa mwana wa dikteta wa zamani ambaye alimuunga mkono sana baba yake hadi kufariki kwake, na ambaye anadaiwa kuchangia pakubwa katika kuagiza mauaji ya waandamanaji. Kwa wengine, wakati mmoja wamwona anafaa kurekebisha serikali na kuwa na nguvu ya kutosha kukomesha machafuko.

Ataungwa mkono au kumpinga?

Kuna orodha ndefu ya wanamgambo, wanasiasa, wafanyabiashara mashuhuri na Walibya wa kawaida ambao watampinga. Baadhi ya Walibya ambao wameteseka tangu baba yake atolewe mamlakani mwaka 2011 wanaweza kumuunga mkono.

Seif al-Islam Gaddafi pia anaweza kuungwa mkono na baadhi ya vikosi vya jeshi na vya kisiasa, wakiongozwa na mwanajeshi, Khalifa Hefter.

Je, anaweza kusafiri nje ya Libya?

Hilo linawezekana. Hata hivyo, bado anatafutwa na Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai ya Hague, ambayo inataka kumfungulia mashtaka kuhusiana na uhalifu wa kivita uliofanywa wakati wa mchafuko wa 2011. Kwa nadharia, kama atasafiri kuelekea nchi yoyote ambayo ni mwanachama wa ICC, nchi hiyo itakuwa na wajibu wa kumkamata.

Dunia itasema nini akirudi madarakani?

Nchi nyingi duniani zilionekana kuchangia kumtoa baba yake madarakani, na ni wazi kuwa Marekani, Uingereza na Ubelgiji havitafurahia. Hata hivyo, kuna imani kati ya Walibya kwamba serikali za Magharibi ziko tayari kufanya kazi na mtu yeyote ambaye angeweza kuleta udhibiti na utulivu nchini, bora tu awe na maoni yanayoambatana na sera zao.

Walibya wamemkumbuka Kanali Gaddafi?

Uongozi wa Gaddafi bado unahusishwa sana na udhalimu na ni wakati ambao Walibya wengi hawapendi kukumbuka. Lakini wengi pia wanahisi kwa sasa uongozi huo ni afadhali kuliko ule wa Gaddafi. Raia wanatamani utulivu na maisha yasiyo na migogoro ambayo inatikisatikisa nchi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles