24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

MTOTO ANAYEISHI KWA KUNYWA MAFUTA, ANA SELIMUNDU – MADAKTARI

NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM


VIPIMO vya awali alivyofanyiwa mtoto Shukuru Kisonga (16) ambaye amekuwa akiishi kwa kunywa mafuta lita moja, maziwa lita mbili na robo tatu ya sukari vimebaini anasumbuliwa na ugonjwa wa selimundu (sickle cell).

Shukuru amefanyiwa uchunguzi huo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), ambako pia amebainika anakabiliwa na upungufu wa madini chuma mwilini.

Daktari bingwa wa magonjwa ya damu wa MNH, Stella Rwezaula, ambaye amemfanyia uchunguzi mtoto huyo, akizungumza na waandishi wa habari jana, alisema hali hiyo ndiyo iliyomsababisha kula vitu hivyo.

“Ripoti niliyopewa awali, inaonyesha Shukuru alishawahi kuletwa hapa Muhimbili Machi mwaka jana na kaka yake, alikuwa akilalamika kupata maumivu na alikuwa anabadilika mara kwa mara, macho yalikuwa ya njano.

“Lakini kabla ya kufanyiwa vipimo, mlezi wake huyo aliomba kuondoka na akaweka saini kwenye faili hilo nililopewa, wakarudi kwao,” alisema.

Alisema hawakurudi tena hospitalini hapo hadi Mei 16, mwaka huu alipopokewa na kulazwa hospitalini hapo na kuanza kufanyiwa vipimo kwa mara ya kwanza.

“Bahati nzuri nilikuwa zamu wiki hiyo, baada ya uchunguzi tumegundua ana tatizo la selimundu, ni ugonjwa ambao amezaliwa nao, amerithi kutoka kwenye vinasaba vya baba na mama yake,” alisema.

Aidha Dk. Rwezaula alisema ugonjwa huo hushambulia chembechembe nyekundu za damu na husababisha kuharibika.

“Badala ya kutengenezwa katika umbo la mviringo, zenyewe hutengenezwa katika umbo la mundu (nusu duara), ndiyo maana unaitwa selimundu.

“Chembechembe hizo zinapogeuka katika umbo hilo la mundu, bandama na viungo vingine vya mwili ambavyo vinahusika na kusaga chembechembe hizo zisizofaa huziharibu na matokeo yake muhusika hupata upungufu wa damu mara kwa mara.

“Kwa sababu zikishasagwa zinatengeneza nyongo na ile nyongo ikiwa kwa kiwango kikubwa mno huwa haiwezi kukaa katika ule mfuko wake ikatosha, hivyo husambaa kwenye sehemu mbalimbali za mwili na ndiyo maana mwili wa mgonjwa hubadilika rangi,” alisema.

Alisema dalili alizokuwa nazo wakati wa utotoni zilidhihirisha tatizo, lakini kwa bahati mbaya wazazi wake hawakuweza kubaini mapema.

“Niliongea na mama yake, akanidokeza kwamba katika kuhangaika kutafuta msaada akiwa hajui tatizo linalomsumbua mwanawe, alikutana na mganga wa tiba mbadala ambaye alimshauri kumpatia vitu hivyo vitatu, ikabidi afuate maelekezo,” alisema.

Alisema hata hivyo uchunguzi umeonyesha kwamba Shukuru alilazimika kutumia kwa wingi vitu hivyo kutokana na upungufu wa madini ya chuma mwilini mwake.

Hata hivyo, daktari huyo alisema hiyo si tiba sahihi kwani wagonjwa wa selimundu hupatiwa vidonge vya folic acid ambavyo huwasaidia kutengeneza damu.

 “Folic acid ni malighafi inayowasaidia kutengeneza damu, kwa sababu damu yao huwa inaharibiwa haraka mno. Kwa kawaida chembechembe nyekundu za damu huishi siku 90 hadi 120 ndipo zinazeeka na kufa.

“Lakini kwa mtu mwenye selimundu huwa zinaishi siku 10, hii inamaanisha kasi ya chembechembe nyekundu kuharibiwa ni kubwa kuliko kasi ya utengenezwaji, ndiyo maana huwa wanahitaji folic acid ili iweze kuwasaidia kutengeneza damu,” alisema.

Dk. Rwezaula alisema wakati mwingine mtu mwenye upungufu wa madini hayo hulazimika kula vitu mbalimbali kama vile magodoro, mkaa, udongo, mchele na kwamba hali hiyo huwakumba zaidi wajawazito.

Alisema tayari wameanza kumpatia vidonge hivyo ambavyo atavitumia maisha yake yote.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles