Na MWANDISHI WETU-SINGIDA
AFYA ya mtoto Mwenge, aliyenusurika kifo baada ya kutumbukizwa chooni na kukaa kwa zaidi ya saa 14 kabla ya kuokolewa akiwa hai, inaendelea kuimarika, huku akiendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Kiomboi, wilayani Iramba.
Mtoto huyo alitupwa chooni na mama yake mzazi, Winfrida Lori (23), ambaye ni mwanafunzi wa Chuo cha Uuguzi cha Kiomboi , wilayani Iramba, ambaye baada ya kubanwa mama huyo alikiri kujifungua mtoto huyo wa kiume katika Kijiji cha Luono, Julai 3, mwaka huu na kisha kumfunga vitambaa mdomoni na kumtumbukiza chooni.
Muuguzi Mkuu wa Hospitali ya Kiomboi, Regina Alex, alisema afya ya mtoto huyo inaendelea kuimarika, pamoja na hali ya mama mzazi wa mtoto, tofauti na hapo awali ambapo alikuwa dhaifu na kushindwa kumnyonyesha mtoto.
“Winifrida alikuwa hawezi kumnyonyesha mtoto Mwenge hapo mwanzoni, lakini sasa hivi anamnyonyesha vizuri na maziwa yanatoka ya kutosha. Mtoto mwenge ana hali nzuri na sasa amefikisha uzito wa kilogramu 2.9, hali ambayo inaridhisha kwakweli,” alisema muuguzi huyo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk. Rehema Nchimbi, ambaye amempa jina mtoto huyo la Mwenge, alisema jina hilo litamfutia mtoto huyo majeraha ya kutupwa chooni na kuwa ishara ya kujiamini, kujipenda, kujithamini na kumpa matumaini kama ambavyo Mwenge wa Uhuru umekuwa ukifanya.
Mkuu huyo wa Mkoa alisema Mwenge wa Uhuru umekuwa ishara ya kuleta matumaini kwa waliokata tamaa, upendo penye chuki na heshima penye dharau na hivyo kitendo cha mama kumtupa mtoto ni kukosekana kwa amani, upendo na heshima katika maisha ya mama huyo.
“Ninamtakia kila la heri mtoto Mwenge ili atakapokuwa alete heshima, upendo na amani katika maisha yake na ya wazazi wake, huku akifuta kumbukumbu mbaya ya maisha yake wakati wa kuzaliwa,” alisema RC Nchimbi.