Na MWANDISHI WETU,
WAZAZI wengi hufurahia kuona watoto wao wakiwa na mwili mkubwa – wakinenepa.
Ili kuhakikisha wananenepa, huhangaika kuwalisha vyakula mbalimbali waonekane wana afya njema. Hii yote ni kwa kwa sababu wanajidanganya kuwa unene ndio afya.
Hawajui ya kuwa ukizidi sana hugeuka na kuwa maradhi. Hebu angalia mfano wa mtoto huyu mwenye miaka 10 aliyezidiwa na mwili hadi kushindwa kumudu masomo.
Namzungumzia mtoto Arya Permana, kutoka nchini Indonesia, ambaye ametajwa kuwa mtoto aliyenenepa zaidi duniani hadi kufikia hatua ya kupewa chakula cha kupunguza uzito.
Permana ameorodheshwa kuwa na unene usio wa kawaida kwa kuwa alikuwa na uzani wa kilo 188.
Awali alilazimika kupumzika kwenda shuleni kwa sababu ya unene wake. Lakini sasa ameweza kuendelea na masomo baada ya kupunguza uzito wa kutosha wa kumwezesha yeye kutembea kwani siku zote alikuwa akilala tu – hakuweza kutembea, hali iliyosababisha kukatisha masomo.
Mtoto huyu alikuwa akila milo mitano kwa siku, lakini baada ya ushauri wa daktari akimtaka kupanga milo na kufanya mazoezi makali, sasa ameanza kupunguza uzito ndani ya wiki chache na anaweza kukaa, kutembea kwenda shule na kucheza na wenzake darasani.