NA VICTOR BARIETY,GEITA
WATU wasiojulikana wamempora mikononi mwa mama yake, mtoto mchanga ambaye ni albino,Yohana Bahati (1), mkazi wa Kitongoji cha Ilyamchele,Kijiji cha Ilelema katika Wilaya ya Chato mkoani Geita na kutokomea naye kusikojulikana.
Katika tukio hilo mama wa mtoto huyo alijeruhiwa kwa mapanga.
Tukio hilo linalohusishwa na imani za ushirikina lilitokea Februari 15 mwaka huu usiku.
Kwa mujibu wa polisi,watu wanaodaiwa kufanya unyama huo walikuwa wawili ambao walivamia nyumbani kwa wazazi wa mtoto huyo wakiwa na mapanga na kutoweka naye kusikojulikana baada ya kuwazidi nguvu wazazi wake.
Kamanda wa Polisi mkoani Geita,Joseph Konyo, alisema tukio hilo lilitokea wakati mama wa mtoto huyo, Ester Jonasi(30), alipokuwa katika harakati za kuandaa chakula cha usiku.
Alisema watu hao wakiwa na mapanga baada ya kufika katika familia hiyo,walimteka mwanamke huyo na katika kunyang’anyana mtoto huyo walimzidi nguvu baada ya kumjeruhi mama huyo kwa mapanga.
Familia hiyo ina watoto watatu wote albino na wakati mtoto huyo anatekwa chini ya himaya ya mama yake mwingine alikuwa kwa jirani anacheza.
“Katika purukushani hizo wahalifu hao walimjeruhi mama wa mtoto huyo mikononi, kichwani na begani na amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Geita kwa matibabu.
“Familia ya mtoto huyo wanaishi eneo la hifadhi ambako hapatakiwi kuishi watu hivyo kutokana na mazingira hayo ilikuwa si rahisi kuwamakata wahalifu hao,”alisema Kamanda Konyo.
Konyo alisema juhudi za wananchi na polisi kufika eneo la tukio hazikuzaa matunda kuwakamata watu hao na jitihada za kuwatafuta watuhumiwa hao zinaendelea.
“Tukio hili ambalo ni la kwanza katika mkoa wetu wa Geita..limetuweka katika mazingira magumu sana, lakini tumejipanga timu ya makachero inaendelea kuchunguza na tutahakikisha huyo mtoto anarudi,” alisema Kamanda.
Alisema baba wa mtoto huyo,Bahati Msalaba, anashikiliwa kwa uchunguzi zaidi kuhusiana na tukio hilo kwa sababu wakati linatokea alikuwa nje anaota moto.
“Tunamshikilia baba wa mtoto kwa sababu ya uchunguzi kwa vile wakati tukio linatokea baba wa mtoto alikuwa nje kwa hiyo kwa uchunguzi wa awali tunamshikilia…Pia mtoto yule mwingine(hakumtaja jina)amechukuliwa na wilaya kwa uangalizi ikizingatiwa eneo hilo lina mazingira magumu,” alisema Konyo.
Hilo ni tukio la pili kutokea katika kipindi kisichozidi miezi miwili ambako Desemba 27 mwaka jana, mtoto Pendo Emanule (4) wa Ndami Misungwi alitekwa na watu wasiojulikana na hadi sasa hajapatikana. Watu waliomteka mtoto huyo nao hawajakamatwa.