26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Mtoto afariki, 30 hoi kwa kula mzoga wa nguruwe

Na Gurian Adolf-Kalambo

MTOTO Mariam Peter (2), amefariki dunia huku watu wengine 30 wakipatiwa matibabu katika Zahanati ya Kalembe Kijiji cha Utengule wilayani Kalambo mkoani Rukwa baada ya kula mzoga wa nguruwe.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Justine Masejo, alisema kuwa Desemba 21, mwaka huu,  Osward Simpungwe alichinja nguruwe ambaye alikuwa amekufa mwenyewe na kisha kuanza kuuza nyama.

Wakazi wa kijiji hicho akiwemo baba wa marehemu walinunua nyama hiyo na kuitumia kwaa jili ya kitoweo, ndipo waliokula nyama hiyo walianza kuugua ugonjwa ambao haukujulikana mara moja.

Kabla ya kufariki mtoto huyo familia nzima walilalamika kuumwa tumbo, ndipo baba yao alipokwenda kwenye duka la dawa muhimu za binaadamu na kununua Flagyl na Panadol na kumpatia mtoto huyo, lakini hata hivyo hazikumsaidia na hali yake ilizidi kuwa mbaya na ilipofika ya saa 10 usiku Desemba 25, alifariki dunia wakati akipelekwa kupatia matibabu katika zahanati ya kijiji.

Mmoja wa wakazi wakazi wa kijiji hicho aliyenusurika baada ya  kula nyama hiyo, Aberi Sinyangwe alisema kuwa katika kijiji chao kumekuwa na uwepo wa matukio ya aina hiyo jambo linalosababishwa na kukosekana kwa maofisa  mifugo ambao wanajukumu la kukagua ubora wa nyama kabla ya kuliwa na binaadamu.

Hata hivyo aliiomba serikali  kupeleka wataalamu  hao kwa ili waondokane  na tatizo la kujirudia  kwa  matukio hayo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa kijiji hicho, Wigani Namsukuma alisema kuwa baada ya serikali ya kijiji kupata taarifa za tukio hilo ilitoa taarifa polisi na kisha kuwakimbiza katika zahanati ya kijiji wagonjwa 30 waliougua baada ya kula nyama hiyo na walipatiwa matibabu lakini kwa bahati mbaya alifariki mtoto huyo. 

Naye Ofisa Mifugo wa Wilaya ya Kalambo,  Enos Luvinga aliwaonya wakazi wa kijiji hicho kuacha tabia ya kula  nyama za mifugo inayojifia yenyewe kwani ni hatari kwa afya zao kwakua mifugo hiyo inakuwa na magonjwa ndiyo maana inajifia yenyewe.

Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kalambo, Rock Sabuni aliwashauri wakazi wa kijiji hicho kuacha tabia ya kujinunulia dawa na kutumia bila kupata ushauri wa daktari, badala yake wanapougua wawe wanakwenda haraka katika zahanati na vituo vya afya kwaajili ya matibabu.

Hata hicho mtuhumiwa aliyeuza mzoga huo wa nguruwe Simpungwe anashikiliwa na polisi kwa mahojiano kutokana na kosa la kuwauzia watu nyama ya mzoga na atafikishwa mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles