24.7 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

MTIKISIKO WA UTALII: WAZIRI WA DK. SHEIN AKAANGWA Z’BAR

Watalii wakiwa visiwani Zanzibar

NA PATRICIA KIMELEMETA-DAR ES SALAAM

SIKU  chache baada ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ),  kutangaza nyongeza ya mshahara wa sekta binafsi  huku wawekezaji wa hoteli wakitishia kupunguza wafanyakazi, Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti wa Baraza la Wawakilish (BLW) amemkangaa Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto, Maudline Cyrus Castico.

Mwenyekiti huyo wa Kamati ya Bajeti, Mohamed Said Dimwa, amesema kamati yake haijashirikishwa kwa mujibu wa sheria katika hatua ya nyongeza hiyo ya mishahara kwa sekta binafsi.

Kauli hiyo aliitoa jana alipozungumza na gazeti hili akisema  kwa mujibu wa utaratibu, kabla Serikali haijafanya jambo lolote la sera, ni lazima kamati yake ishirikishwe na iridhie ama laa.

“Serikali imeshindwa kuwasilisha mapendekezo kwenye Kamati ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi,  badala yake Waziri amekaa na watendaji wake na kuamua kuongeza kima hicho  jambo ambalo limetufanya tusome taarifa hiyo kwenye vyombo vya habari,” alisema Dimwa.

Alisema suala hilo ni la kushangaza kwa sababu  kamati yake  haijui lolote kuhusu nyongeza hiyo.

Alisema   sheria inatambua kwamba kila ongezeko la fedha lazima lipitie kwenye kamati hiyo lakini ongezeko la kima cha chini sekta ya utalii halikupitishwa kwenye kamati, jambo ambalo limechangia kujitokeza   malalamiko mengi kutoka kwa wawekezaji wa sekta hiyo.

Mohamed alisema Serikali inapaswa kuliangalia upya suala hilo na kulifanyia kazi   kupunguza malalamiko hayo ambayo yanaweza kuathiri sekta ya utalii ikiwamo Wazanzibari kukosa kazi.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Jumuiya ya Wawekezaji Sekta ya Utalii Zanzibar (ZATI), Seif Masoud Misri, alisema ongezeko hilo linaweza kuathiri sekta ya utalii kwa sababu  baadhi ya makampuni yamepanga kupunguza wafanyakazi.

Alisema serikali ilitoa notisi hiyo wiki mbili zilizopita na kuwataka waajiri kuongeza mishahara ndani ya kipindi hicho bila kuwashirikisha katika  uamuzi huo.

“Tumeshangazwa na serikali kuongeza kima cha chini cha mishahara kwenye sekta ya utalii bila  kutushirikisha jambo ambalo limechangia baadhi ya makampuni ya utalii Zanzibar kupanga kupunguza wafanyakazi,” alisema Masoud.

Alisema kitendo cha serikali kuongeza Sh 300,000 kwa kima cha chini cha mshahara ikijumlishwa na kodi, nyumba na michango ya mifuko ya jamii ikiwamo ZSSF, mtu mmoja anaweza kulipwa   zaidi ya Sh 500,000.

Alisema   pia kuwa bado hata wafanyakazi waliowaajiri hulazimika kuwalipia nyumba, matibabu na kwa   mishahara  hiyo iliyoongezwa kwa asilimia 109 inafanya   washindwe kuwa na kiwango kikubwa cha wafanyakazi.

“Mchakato wenyewe wa kuongeza mshahara hatujashirikilishwa. Lakini pia  tumepewa notisi ya wiki mbili  tuanze kutekeleza jambo ambalo limechangia kujitokeza   malalamiko,” alisema.

Alisema sekta hiyo imekua ikichangia uchumi wa Zanzibar kwa asilimia saba  kwa mwaka  hali ambayo kwa sasa inaweza kuathiri na kushusha mapato ikiwa wafanyakazi wa sekta hiyo watapungua.

Alisema   serikali ya Zanzibar inapaswa kuliangalia suala hilo na kulifanyia kazi.

Akizungumzia hali hiyo, Waziri Ofisi ya Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Abood, alisema ofisi yake imesikia kilio cha wawekezaji hao wa sekta ya utalii.

Alisema  tayari waziri mwenye dhamana ameingilia kati na ameanza kulifanyia kazi suala hilo.

Waziri alisema anachofahamu kwa sasa ni kwamba watu wanaolalamikia hali hiyo wamekwisha kuandika barua ya malalamiko na anaamini kilio chao kitafanyiwa kazi na Serikali kwa wakati.

“Ni kweli kumekuwa na malalamiko katika suala hili lakini uzuri ni kwamba walalamikaji tayari wamewasilisha barua kwa waziri mwenye dhamana  kuangalia namna ya kulishughulia.

“Kutokana na hali hiyo, ofisi yangu inasubiri uamuzi wa waziri  tuweze kuyafanyia kazi,” alisema Abood.

Mwenyekiti, Kamati ya  Wenyeviti wa Kamati za Kudumu, Hamza Hassan Juma, alisema kamati yake inashughulikia masuala ya utalii lakini kwa  suala linalohusu mishahara lipo chini ya Kamati ya Bajeti.

“Suala la mishahara linasimamiwa na kamati ya bajeti siyo kamati yangu hivyo basi malalamiko hayo hayahusu kamati yangu moja kwa moja,” alisema.

Akijibu malalamiko hayo, Naibu Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto, Shadya Mohamed Suleiman alisema   kabla ya kupitishwa  ongezeko hilo, wizara yake ilikutana na wadau mbalimbali na kulijadili.

“Unajua hili suala limegusa masilahi ya watu ndiyo maana wametugeuka na kudai hatujawashirikisha wakati siyo kweli.

“Hatuwezi kukurupuka kutekeleza majukumu yetu wakati sheria tunajua,” alisema Shadya.

Alisema katika vikao vya majadiliano kuna baadhi ya wadau walifika  wenyewe na wengine walituma wawakilishi wao na kutoa maoni yao ya nini kifanyike   kuhakikisha wanaboresha mishahara katika sekta ya utalii.

Alisema  baada ya kuanza kutekeleza makubaliano yao ndipo yalipojitokeza maneno hayo wakati suala lote wanalifahamu.

“Waziri hawezi kukurupuka na  kutangaza ongezeko hili kabla ya kushirikisha wadau.

“Kinachofanyika sasa ni kutugeuka wakati suala zima wanalifahamu, tumeshangazwa sana,” alisema.

Alimtaka mwandishi wa habari   kwenda ofisini kwake  kuzungumza suala hilo pomoja na kumpa vielelezo.

Ongezeko hilo lilitangazwa na Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto, Maudline Cyrus Castico ambaye alisema kuwa kima cha chini ya mishahara   ni Sh 300,000 bila ya kodi na mifuko ya hifadhi ya jamii(ZSSF).

Waziri  pia alitangaza mishahara mipya kwa sekta binafsi ambako  kima cha chini kilikua Sh 145,000 hadi Sh 180,000.

Alisema mabadiliko hayo yamefanyika kwa mujibu wa  kifungu cha 97(1) cha Sheria ya Ajira Namba 11 ya Mwaka 2005.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, wadau   walisema   ongezeko hilo  halijawasilisha kwenye Kamati ya Bajeti ya Bunge la Baraza la Wawakilishi na kwamba wamesoma taarifa hiyo kwenye vyombo vya habari.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles