31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

MTIKISIKO ACACIA, KIGOGO WAKE AKAMATWA

Na Mwandishi Wetu-DAR ES SALAAM


KAMPUNI ya Uchimbaji Madini ya Dhahabu ya Acacia imepata mtikisiko baada ya Makamu wake wa Rais nchini, Deo Mwanyika, kukamatwa na baadae kuachiwa, MTANZANIA limedokezwa.

Mbali na kukamatwa kwa Mwanyika, mmoja wa wajumbe wa bodi ya kampuni hiyo, Balozi Juma Mwapachu, ameomba kustaafu.

Hatua hiyo inakuja wakati mazungumzo kati ya Serikali na Kampuni ya Barrick Gold Corporation ya Canada juu ya sakata la mchanga wa dhahabu (makinikia), yakitaratajiwa kuanza hivi karibuni.

Chanzo cha kuaminika kimelidokeza gazeti hili kuwa, Mwanyika alikamatwa na vyombo vya dola juzi na baadae kuhojiwa, huku hati yake ya kusafiria na vifaa vyake vya mawasiliano vikishikiliwa.

Chanzo kingine cha habari kilieleza kuwa, Mwanyika alikamatwa akiwa Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere Dar es Salaam.

Kutokana na hali hiyo MTANZANIA ilimtafuta Msemaji wa Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa Tanzania (Takukuru) ili kuzunguzia suala hilo.

Alipopigiwa simu yake iliita muda mrefu bila kupokewa hadi tunakwenda mitamboni. Hata hivyo taarifa ya Acacia ilisema.

“Deo Mwanyika Makamu wa Rais wa Acacia wa Masuala ya Shirika hajakamatwa wala hashikiliwi nchini Tanzania. Acacia inaendesha shughuli kwa uwazi na inakana tuhuma zozote za kuficha kiwango cha mapato ili kukwepa kulipa kodi stahili na inatoa ushirikiano kwa uchunguzi unaoendeshwa na Serikali ya Tanzania kuhusu tuhuma hizo,” ilisema.

Juni 12, mwaka huu Rais Dk. John Magufuli, alikabidhiwa ripoti ya pili ya mchanga wa madini iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa tume hiyo, Profesa Nehemiah Osoro.

Kutokana na hali hiyo Kampuni ya Acacia ilieleza kushangazwa na matokeo ya ripoti  hiyo.

Taarifa iliyotolewa na Acacia   kupitia tovuti yake, saa chache baada ya ripoti hiyo kusomwa na Profesa Osoro, ilisema kampuni hiyo imesikitishwa na ripoti ya kamati ambayo ni historia katika uchumi wa nchi hii na mambo ya sheria ya kusafirisha mchanga wa madini.

Kwa mujibu wa Acacia,  ripoti ya pili imejikita katika matokeo ya ripoti ya kwanza iliyotolewa Mei 24 mwaka huu ambayo kampuni hiyo imekuwa ikiipinga vikali.

Taarifa hiyo inasema ripoti hiyo ilihusisha matokeo ya sampuli za makotena 44. Acacia ilisema kwa taarifa zake za miaka zaidi ya 20 ni vigumu kupatanisha matokeo hayo ambayo yametaja kiwango kikubwa cha thamani ya zaidi ya mara 10.

Kwa mujibu wa ripoti iliyowasilishwa na kamati ya pili hiyo jana,   Acacia haijawahi kutangaza mapato na kulipa kodi kwa kipindi cha miaka mingi ambayo ni mabilioni ya dola za Marekani.

Taarifa ya kampuni pia inadai kwamba ripoti ya pili inaishutumu Acacia kutoonesha mapato halisi pamoja  kutolipa kodi ya mabilioni ya dola za Marekani.

Kwa matokeo hayo, kamati hiyo imetoa mapendekezo ya kuitaka Acacia ilipe kiasi chote cha kodi inachodaiwa, kufanya mazungumzo ya makubaliano ya uchimbaji wa madini, umiliki wa Serikali katika migodi na muendelezo wa kupiga marufuku usafirishaji nje   mchanga wa madini.

“Acacia inakanusha madai haya mapya na ushahidi wake. Sisi tunafanya biashara kwa viwango vya juu  na kufuata sheria zote za Tanzania.

“Tunarudia tena kwamba tulitangaza kila kitu tulichozalisha katika thamani ya  biashara tangu tulipoanza kazi Tanzania na tumelipa mirahaba na kodi ya madini tuliyozalisha,” ilisema taarifa hiyo.

Taarifa hiyo iliongeza kuwa. “Kwa muda mrefu tumekuwa tukishirikiana na Serikali na tunaamini kwamba tuna malengo sawa katika kuimarisha maendeleo ya  jamii na uchumi nchini Tanzania.

“Acacia inabakia wazi   kuendeleza mazungumzo na Serikali juu ya suala hili na tunaendelea kutathmini yote yaliyoibuliwa na ripoti,” ilieleza taarifa hiyo ya Acacia.

Balozi Mwapachu astaafu

Wakati hayo yakiendelea mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni ya uchimbaji ya Acacia, Balozi Juma Mwapachu ametangaza kustaafu nafasi hiyo baada ya kuitumikia kwa vipindi viwili.

Mwapachu alitangaza uamuzi huo jana baada ya muhula wake wa pili wa miaka mitatu mitatu wa ujumbe wa bodi hiyo, kumalizika.

Taarifa iliyotumwa na Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti ya Acacia imemshukuru Balozi Mwapachu kwa utendaji wake na ushirikiano wake wote  alipokuwa mjumbe.

“Tunamtakia maisha mema,” ilielza taarifa hiyo.

Kutokana na mabadiliko hayo, Bodi ya Acacia itabaki na wajumbe saba, wakiwamo wakurugenzi wane na wasio kuwa wakurugenzi.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles