NA Waandishi Wetu, Chalinze na Dar
MWANASIASA mkongwe na Mwenyekiti wa Chama Cha Democratic (DP), Mchungaji Christopher Mtikila (62) amefariki dunia kwa ajali ya gari katika Kijiji cha Msolwa, Jimbo la Chalinze mkoani Pwani, barabara Kuu ya Morogoro.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Pwani, Jafary Ibrahimu alisema ajali hiyo ilitokea saa 11 alfajiri usiku wa kuamkia jana alipokuwa akitoka mkoani Njombe kurejea Dar es Salaam.
“Ni kweli Mtikila amefariki dunia saa 11 alfajiri katika eneo la Msolwa karibu na mjini wa Chalinze lakini kifo chake kimesababishwa na ajali ya gari lililoacha njia na kupinduka kutokana na mwendo kasi,”alisema Kamanda Ibrahimu
Alisema Mtikila ambaye ni mkazi wa Mikocheni B Dar es Salaam alikuwa na wenzake watatu katika gari ya Toyota Corola ambayo ilipofika eneo la tukio iliacha njia na kuingia porini umbali wa mita 200 hali iliyosababisha tairi ya mbele kushoto kupasuka na kupinduka na kusababisha kifo cha Mtikila huku wenzake watatu wakijeruhiwa.
Kamanda alisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi na kwamba ilitokea kwenye eneo ambalo siyo makazi ya watu jambo lilisababisha waliopatwa na ajali kukosa msaada wa haraka.
Aliwataja waliojeruhiwa kuwa ni Mchungaji Patrick Mgaya (37), Ally Mohammed (42) wote wakazi wa Dar es Salaam.
Alisema polisi wanamshikilia dereva wa gari hilo, George Stephen (31) maarufu kama Ponela mkazi wa Dar es Salaam kwa mahojiano zaidi.
Kamanda Ibrahim alisema mwili wa marehemu Mtikila ulihifadhiwa katika Hospitali ya Tumbi na majeruhi wanaendelea na matibabu katika hospitali hiyo.
Baadhi ya wananchi walioshuhudia tukio hilo walisema gari hilo lilikua kwenye mwendokasi wakati linalipita kijiji Msolwa.
“Wakati gari hii inapita kijijini Msolwa alfajiri ya leo (jana) lilikua kwenye mwendo kasi sana hali iliyosababisha ajali hiyo,”alisema Mussa Omary mkazi wa kijiji hicho.
Mmoja wa majeruhi, Mchungaji Patrick Mgaya alipata matibabu katika Hospitali ya Tumbi na kuruhusiwa kwa vile kuwa hali yake ilikuwa inaendelea vizuri.
Kwa mujibu wa Mgaya, walitoka Njombe walkokuwa wakimnadi mmoja wa wagombea ubunge ambaye hakutaka kumtaja.
Alisema walipomaliza mkutano wa kampeni walipumzika kabla ya kuanza safiri ya kurejea Dar es Salaam.
Mchungaji Mgaya alisema wakati wanapanga kurudi Dar es Salaam hawakuwa na usafiri hivyo walilazimika kukodi gari ya George (aliyekuwa dereva wa gari hilo) na kuanza safari usiku.
Alisema walipofika karibu na eneo la ajali waliona dereva anaongeza mwendo na wao wakamwambia apunguze na ndipo muda mfupi baadaye waliona gari linaanza kuyumba na kupoteza muelekeo hali ambayo iliyosababisha liache njia na kupinduka.
Mgaya alisema muda mmfupi baada ya ajali hiyo walitokea a wasamaria wema ambao waliwasaidia kuwaokoa kabla ya kutokea polisi kutoka Chalinze ambao waliwachukua na kuwapeleka katika Kituo cha Afya Chalinze na wengine katika Hospitali ya Tumbi.
Hata hivyo alisema wakati wanatolewa katika gari, Mchungaji Mtikila alikuwa tayari amefariki dunia huku Mohamed Ally akiwa katika hali mbaya.
Mfanyakazi mmoja wa chumba cha maiti katika Hospitali ya Tumbi ambaye hakutaka jina lake litajwe, alisema wa alipokea mwili wa Mtikila ambaye alionekana ameumia kidogo kichwani na kiunoni na hakuwa na majeraha makubwa.
“Niliona mwili wa Mtikila nikiwa chumba cha maiti lakini majeraha yake ni madogo kwa sababu aliumia kidogo kichwani na mgongoni lakini aliyeumia sana na yule Ally Mohamed,”alisema mfanyakazi huyo.
Kamanda Ibrahim alisema uchunguzi zaidi wa ajali hiyo unaendelea na taarifa zitaendelea kutolewa huku akitoa pole kwa familia ya Mchungaji Mtikila katika kipindi hiki kigumu.
Aliwataka madereva kuwa makini wanapokuwa barabarani na wazingatie sheria ikiwamo kutumia mwendo ambao ni salama kwao na abiria wao.
Nyumbani kwa Mtikila
MTANZANIA jana ilifika nyumbani kwa marehemu Mtikila, Mikocheni B Dar es Salaam na kushuhudia watu wengi wakiwamo viongozi wa serikali wakiomboleza na kuwapa pole wafiwa.
Akizungumzia alivyopokea msiba huo, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi alisema amepoteza mdau wa siasa na ameshtushwa na kifo hicho ambacho kitawakutanisha watu wengi hivyo kitumike kama njia moja ya kusambaza amani.
Naye Katibu Mwenezi wa Chama cha DP, Mshambichake Ferouz, alisema chama hicho kimepokea msiba huo kwa masikitiko makubwa na pengo lake halizibiki kwa vile alikuwa mstari wa mbele kuhakikiksha chama hicho kinasonga mbele.
Habari hii imeandikwa na GUSTAPHU HAULE na Patricia Kimelemeta, Chalinze na Mauli Muyenjwa, Dar es Salaam