Na THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM
KATIKA kuhakikisha inazidi kujiweka imara, timu ya Mtibwa Sugar ina mpango wa kucheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Yanga, kwa ajili ya kujiandaa na msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Katika mchezo wa kirafiki uliopita Mtibwa walifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mbeya City, mchezo uliopigwa Uwanja wa Jamhuri Morogoro wikiendi iliyopita.
Akizungumza na MTANZANIA jana Ofisa Habari wa klabu hiyo, Thobias Kifaru, alisema wanataka kukiimarisha kikosi chao vizuri kupitia mechi hizo ambapo kwa sasa wapo katika maandalizi ya kukutana na timu hiyo.
“Mchezo uliopita tulifanikiwa kupata ushindi hivyo tutaendelea kujipima zaidi kwa mechi nyingine ambazo zitamsaidia kocha kufahamu mapungufu yaliyopo katika kikosi na kuyafanyia kazi, tunajipanga wiki hii mwishoni kucheza na Yanga japo hatujajua siku,” alisema.
Alisema bado wanaendelea na usajili kwa wachezaji wengine ambao wataona watailetea timu hiyo matokeo mazuri na kuzidisha ushindani katika msimu ujao wa Ligi Kuu.