NEW YORK, Marekani
UTAWALA wa Rais Donald Trump, umezidi kuandamwa na malalamiko kuhusu vitendo vya unyanyasaji kijinsia, baada ya mwanamke wa pili kujitokeza akidai kufanyiwa kitendo hicho na mteule wa kiongozi huyo katika Mahakama Kuu ya nchi hii, Brett Kavanaugh.
Taarifa zilizopatikana mjini hapa jana zilieleza kwamba, mwanamke huyo, Deborah Ramirez, ambaye alisoma na jaji huyo katika Chuo Kikuu cha Yale aliiambia mahakama hiyo kwamba, Kavanaugh alimwonesha sehemu zake za siri wakati wakiwa bwenini madai ambayo yanakanushwa na jaji huyo.
Katika malalamiko hayo, Ramirez, anadai kwamba tukio hilo lilitokea wakati akiwa binti na wakati huo wakisoma pamoja na jaji huyo katika Chuo hicho kikuu mwaka 1983-4.
Alisema wakati anafanyiwa kitendo hicho walikuwa wakishiriki katika mchezo wa kunywa ambapo watu wengine walikuwa wamekaa kwenye mduara wakiwaangalia.
“Nakumbuka nilielekezewa uume mbele yangu,” alisema mwanamke huyo. “Nilikuwa nafahamu si kitu ambacho nilikipenda na kiliniumiza sana akili,” aliongeza.
Ramirez alisema mbali na kuoneshwa sehemu hiyo ya siri, alidhihakiwa na kutukanwa wakati aliposema kuwa hakutaka kufanyiwa hivyo na baadaye akaishia kugusa sehemu za siri za kiume wakati akijaribu kumsukuma mwanamume huyo.
Tuhuma dhidi ya jaji huyo zimekuja zikiwa ni hatua za mwisho kwa kigogo huyo kukabidhiwa madaraka rasmi ambapo anatakiwa kupitishwa na maseneta wa Kamati ya Wanasheria kabla ya jina lake kukabidhiwa mikononi mwa baraza zima la maseneta.
Kwa upande wake mlalamikaji wa kwanza, Profesa Christine Blasey Ford, ambaye wiki iliyopita ndiye aliyekuwa wa kwanza kuwasilisha malalamiko yake dhidi ya Kavanaugh kuhusu kufanyiwa ukatili huo kijinsia miaka ya 1980, ameshakubali kuwasilisha ushahidi wake katika baraza hilo la maseneta Alhamisi wiki hii.