Na Clara Matimo, Mwanza
Taasisi ya Mtembezi Adventures inayojihusisha kuratibu na kuandaa shughuli mbalimbali zenye lengo la kuhamasisha utalii wa ndani imepanga kutumia mbio za Mtembezi zilizopangwa kufanyika Oktoba 29, mwaka huu jijini Mwanza kwa ajili ya kuhamasisha utalii ukiwamo wa miamba.
Hayo yamebainishwa Oktoba Mosi, 2023 jijini hapa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mtembezi Adventures, Samson Samwel alipozungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi rasmi wa mbio hizo.
Amesema wameamua kuhamasisha utalii wa vivutio mbalimbali vilivyomo mkoani Mwanza baada ya kubaini katika jamii nyingi kuna dhana kwamba utalii unafanywa na watu wenye kipato kikubwa.
“Taasisi ya Mtembezi Adventures tunatamani jamii ielewe kwamba mtu yeyote anaweza kufanya utalii kwa sababu una tija katika maendeleo ya nchi yetu, tunatamani kuona utalii unakuwa sehemu ya utamaduni wa jamii zetu maana utalii ni moja ya sekta ambazo zinautajiri wa vitu vingi ndani yake ikiwemo miamba.
“Hivyo, ndiyo sababu tumekuja Mwanza kuhamasisha utalii uliopo ndani ya mkoa huu ikiwa ni pamoja na jiwe la Bismarck ambapo wataalamu wa miamba watatuelezea zaidi ili watu wapate kufika kwenye maeneo hayo na kujifunza zaidi,” amesema Samwel.
Kwa mujibu wa Mkurugezni huyo wa Mtembezi Adventures mpaka sasa maandalizi ya mbio hizo zenye lengo la kuwakutanisha watu wasiopungua 1,000 yamefikia asilimia 35, nakwamba wanaendelea na utaratibu mwingine wa kiitifaki ili kupata ubora wanaoutaka.
Amefafanua kwamba taasisi hiyo ndiyo inayoratibu mbio hizo za kilometa 21, 10, 5 na 2.5, ikishirikiana na wafadhili mbalimbali wakiwemo The Cask Bar & Grill ambako pia tiketi zinapatikana kwa gharama ya Sh 40,000, Kampuni ya Don resources (T) Co. Ltd na Mwanza Hospital huku akiweka wazi kwamba bado milango iko wazi kwa wadau wengine watakaohitaji kushirikiana nao kwenye mbio hizo.
“Mbio za kilomita mbili ni kwa ajili ya watoto, utofauti mkubwa kati ya marathon zetu na zingine sisi tunafanya kwa ubora zaidi na tuna ujumbe ambao utanufaisha wananchi wa kada mbalimbali na umri tofautitofauti siku hiyo ya Oktoba 29, 2023 tukio letu litaanza na kuishia katika viwanja vya baada ya The Cask.
“Tumejipanga kuwaalika baadhi ya wasanii na watu mashuhuri kuja kushiriki na sisi kwenye Mtembezi Marathon Mwanza 2023 majina yao tutayaweka wazi baada ya siku chache kuanzia leo lengo ni kuhamasisha utalii wa ndani kupitia michezo, kuwaleta pamoja wadau wa utalii ili kufikisha ujumbe kwa wananchi wajue mchango wa utalii kwenye maendeleo,” ameeleza Samwel.
Meneja Miradi wa Taasisi ya Mtembezi Adventures Yussrah Bori amesema Mtembezi Marathon imekwishafanyika katika mikoa mbalimbali ikiwemo Dar es Salaam, Dodoma, Kigoma, Tabora na mwaka huu 2023 inatarajia kufanyika Mwanza.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Don resources (T) Co. Ltd, inayojihusisha na utafiti wa madini, uchimbaji, ujenzi wa miundombinu sekta ya madini, kusambaza vifaa na mavazi yanayohusisha kazi za uchimbaji na utafiti wa madini, Mukhusin Kikulu amesema wamevutiwa kudhamini mbio hizo ili kutimiza lengo lao la kufanya ushawishi kwa jamii na Serikali katika utalii wa miamba.
“Tumevutiwa kushiriki katika udhamini wa mbio hizi kwa sababu ya kuvutiwa na kipengele cha utalii maana nasisi kwenye sekta ya madini tunakipengele kikubwa sana cha utalii kinachofahamika kama Geo Tourism,” amesema na kufafanua zaidi kuwa:
“Geo Tourism inatengenezwa na Geological Features ambazo ni miamba, iko miamba ambayo ukiiona unavutiwa kuitazama namna ambavyo imetengenezwa, imeathirika au mazingira yake, mbali na kuwa na madini lakini miamba tu inaweza ikakuvutia na ukafanya utalii kwa hapa jijini Mwanza mlima Bismarck ni miongoni mwa maeneo hayo,” ameeleza Kikulu ambaye pia ni Mwanajiolojia.
Naye Meneja Mwendeshaji wa The Cask Bar & Grill Samwel Mwaifwani amesema wanafuraha kuwa wadhamini wakuu wa Mtembezi Marathoni 2023, Mwanza sababu wanaamini kuwa mbio hizo ni fursa muhimu ya kuhamasisha utalii wa ndani na kujenga afya ya jamii.
“Mwanza ni mji mzuri wenye vivutio vingi vya asili na kihistoria, tunaamini mbio hizi zitasaidia kuvutia wageni kutoka ndani na nje ya nchi kuja kutalii ndani ya mji wetu huu, tunaamini kwamba mbio hizi zitakuwa na mafanikio makubwa hivyo tutaendelea kuunga mkono michezo hapa nchini.
“Tunapenda kuhamasisha Watanzania kushiriki mbio hizi zitakazofanyika katika mkoa wa Mwanza ili kufanya mazoezi na kuboresha afya zao pia kwa kufanya hivyo watakuwa wameshiriki kuvutia wageni kutoka ndani na nje ya nchi kuja kutalii ndani ya mji wetu ili kuuingizia kipato,” amesema Mwaifwani.