Na Mwandishi Wetu-DAR ES SALAAM
BAADA ya kubainika nguvu kazi ya Taifa hasa vijana inateketea kutokana na matumizi ya dawa za kulevya, Januari 4, mwaka huu gazeti hili lilikuwa la kwanza kujitosa kufichua hali hiyo, jambo ambalo limesaidia mamlaka husika kuanza kuchukua hatua ya kupambana kwa vitendo.
Kwa mujibu utafiti uliofanywa na gazeti hili, ilibainika kuwa kundi kubwa la vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 30 limekuwa likiteketea kutokana na matumizi ya dawa za kulevya.
Kundi la wasanii wa muziki wa kizazi kipya na vijana wa kimasikini wamekuwa ni waathirika wakubwa hali inayotishia nguvu kazi ya Taifa.
Kwamba kundi hilo la wasanii sasa limegeuka mateka, huku hali hiyo ikichangiwa na wafanyabiashara wakubwa, ambao wamekuwa wakiwashawishi kwa fedha na hata kuwahonga magari ili waweze kutumia mihadarati.
MTANZANIA ilizungumza na baadhi ya wasanii ambao wamejikuta katika matumizi ya mihadarati hiyo na hata kuonekana kuwaumiza, huku wengine wakiwa kama wendawazimu.